Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima ameitaka timu ya Mtibwa Sugar kuongeza juhudi katika ligi kuu ya Tanzania bara (NBC premier league) ili kusalia katika ligi hiyo kwani ina wachezaji wazoefu, mahili na wenye nidhamu huku akihimiza umoja na ushirikiano ndani ya timu hiyo.
Mhe. Malima amesema hayo alipoitembelea timu hiyo iliyopo Wilayani Mvomero akiwa na lengo la kutatua changamoto zinazoikabili na kuongeza hamasa ya mchezo wa mpira wa miguu Mkoani Morogoro.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa yeye akiwa kama mlezi wa timu hiyo ameamua kuchukua hatua za mapema ili kuinusuru timu kubaki ligi kuu msimu wa 2023/2024 na kwamba hatoifumbia macho timu hiyo ikifanya vibaya kwani ndio timu pekee inayoshiriki ligi kuu Mkoani Morogoro.
"... sasa ukishakuwa mlezi wa timu maana yake haiwezekani mambo yakawa yanaharibika nawe unayaangalia tu, tumekubaliana tufanye tathmini ya sasa ya Mtibwa tumeshabaini vitu vingi sana ambavyo vitarekebishwa na kuirejesha timu nafasi nzuri..."
Pia, Mhe. Adam Malima amesikitishwa na timu hiyo kushika nafasi ya mwisho kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara kwani amesema ina wachezaji wazuri na wazoefu wa mashindano hayo, hivyo ziara ya kiongozi huyo itakuwa na tija katika kuinusuru timu hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima ameuagiza uongozi wa Mtibwa Sugsr kuwa na uongozi imara na wenye ushirikiano baina ya benchi la ufundi sambamba na wachezaji kwa manufaa ya timu yenyewe na Mkoa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amesema Mkoa wa Morogoro una timu moja inayocheza ligi kuu ambayo ni Mtibwa Sugar na kukiri kwamba timu hiyo ipo katika hali mbaya misimu mitatu mfululizo hivyo Viongozi wamechukua hatua za mapema katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili timu hiyo.
Naye Kocha Mkuu wa Timu ya Mtibwa Sugar Zuber Katwila kwa niaba ya benchi la ufundi amesema timu hiyo ipo katika mapambano ya kutafuta alama 12-14 muhimu katika mzunguko wa kwanza ili kujiweka katika nafasi nzuri na kumshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kuhamasisha na kuchagiza maendeleo ya timu hiyo ambayo ndio timu pekee Mkoani Morogoro.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.