Bodi ya Wakala ya Nishati ya umeme Vijijini (REA) imepanga kumchukulia hatua kwa kumsimamisha kazi Mkandarasi wa Kampuni ya HNXJDL kutoka nchini China kwa kushindwa kukamilisha mradi wa kuunganisha umeme katika Vijiji 146 Mkoani humo Morogoro.
Kauli hiyo imetolewa Januari 26 mwaka huu na Bwana Styden Rwebangila Mjumbe wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) baada ya kikao kilichowakutanisha wadau wa nishati Mkoani Morogoro wakiwemo Wabunge wa Mkoa huo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mjumbe wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Styden Rwebangila, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao.
Bwana Rwebangila amesema Mkandarasi huyo alipewa tenda ya kukamilisha mradi wa kuunganisha umeme katika Vijiji 146 ambapo Vijiji 36 pekee amekamilisha huku muda wa kukabidhi mradi huo ni Februari 18, 2023.
Aidha, baada ya majadiliano na wajumbe wa kikao hicho wameazimia kumpunguzia maeneo ya mradi huo kwa kuyagawa kwa wakandarasi wengine na kumtaka Mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo kwa wakati katika maeneo machache aliyobaki nayo.
“...kumpunguzia kazi angalau asilimia 50 ili aweze kubaki na Vijiji vichache na wananchi wapate umeme kama Serikali ilivyo kusudia”. amesema Bwana Rwebangila.
Sambamba na hilo Bwana Rwebangila amesema Serikali imeamua kuongeza vigezo kwenye utoaji wa tenda kwa wakandarasi kwa lengo la kuwapata wakandarasi wenye sifa na uzoefu wa kukamilisha miradi yao kwa wakati.
Kwa upande wake Mbuge wa Mikumi na Katibu wa Wabunge Mkoa wa Morogoro Mhe. Denis Londo amesema kwa muda mrefu wananchi katika Jimbo lake wanamlalamikia kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi ya kuhakikisha kuwa kila kijiji ndani ya Jimbo hilo kinapata huduma ya umeme.
Mhe. Denis Londo Mbunge wa Mikumi akielezea kutokufurahishwa na kasi ya Mkandarasi ya kutekeleza Miradi ya umeme katika Jimbo lake.
Aidha, Mhe. Londo amesema hawakubaliani na kasi ya Mkandarasi huyo katika kutekeleza kazi yake ndani ya Jimbo hilo hivyo kupitia kikao hicho wamekubaliana kumpunguzia maeneo ya mradi huo kutokana na kuchukua maeneo mengi na kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati kama mkataba unavyoelekeza.
Nae Mbunge wa Malinyi Mhe. Antipas Mgungusi ameishukuru Serikali kwa kuunganisha umeme katika Jimbo lake ambapo kati ya Vijiji 33, Vijiji 32 vimeshaunganishwa na umeme kwa awamu ya kwanza na wanatarajia mradi wa Ujazilizi ambapo vitongoji vyote ndani ya Wilaya hiyo vitaunganishwa na huduma ya umeme.
Mradi huo wa kuunganisha umeme awamu ya tatu katika Mkoa huo ulikuwa unatekelezwa na Wakandarasi wawili ambapo Mkandarasi wa Kampuni ya STEG tayari imekamilisha miradi yake kwenye Vijiji 83 katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Miradi hiyo ya kuunganisha umeme Mkoani Morogoro unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 71.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.