Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslimu amesema moja ya sababu kubwa zinazopelekea uhalifu kuendelea kuwepo ndani ya jamii ni wananchi kuogopa kulaumiwa kwa kuwataja wahalifu ambao wanaishi miongoni mwao.
Kamanda Muslimu ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipoambatana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela kwenye ziara ya siku moja Wilayani Kilosa kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi ikiwemo migogoro baina ya wakulima na wafugaji inayolalamikiwa na wananchi wengi wa Wilaya hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslimu (wa kwanza kulia) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chanzuru.
Amebainisha kuwa wahalifu wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya kihalifu mara nyingi hawatoki mbali na jamii husika bali wapo miongoni mwao na wanafahamika ambao ni kaka, dada, baba, na shangazi, tatizo kubwa la jamii yetu ni kuogopa kutajana na kuhofia lawama.
“Wengine ni marafiki zetu, sasa tumekuwa na ugonjwa mbaya sana na ugonjwa huu unatuumiza vibaya sana, tunaogopa lawama, tunaogopa kuwataja wahalifu ili wachukuliwe hatua” amesema Kamanda Muslim.
Katika hatua nyingine Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro ameapa kutofumbia macho suala la baadhi ya wafugaji kulishia mifugo yao katika mazao ya wakulima kwa makusudi na kusababisha kero kwa wengine.
Akibainisha lengo la kukomesha tabia hiyo kwa wafugaji wasiotii sheria na kusababisha umaskini kwa wengine amesema ataungana na Mwenyekiti wake wa Kamati ya Ulinzi na Uslama ya Mkoa ambaye pia ndiye Mkuu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya kuhakikisha anakomesha tabia hiyo.
Akithibitisha kauli hiyo kwa vitendo, Kamanda Muslim amemuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Tarafa ya Kimamba kuwakamata mara moja watuhumiwa wawili ambao wanadaiwa kulishia mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na kukataa kulipa fidia ya uhalibifu wa mazao hayo yaliyotathminiwa na Afisa kilimo.
“… OCS chukua taarifa za huyo mama aliyelishiwa mazao yake na mimi nitakapoondoka hapa kabla sijafika Morogoro awekwe ndani, na asitoke ndani mpaka amlipe mama pesa yake…” amesema Kamanda Muslim.
Kwa upande wao wahanga wa tukio hilo akiwemo Bi. Juliana William Matei Mkazi wa kijiji cha Chanzuru amemlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuwa ananyanyaswa na baadhi ya wafugaji jamii ya wamasai kwa kulishiwa mazao yake mifugo na hawataki kulipa fidia iliyotathminiwa na Afisa Kilimo ambayo ni Tsh. 285,000 huku wao wakitaka kumlipa Tsh. 20,000/= pekee.
‘’….Mhe. Mkuu wa Mkoa, mwaka huu mimi nimelimia ng’ombe toka mwezi wa nne nahangaika na kesi ya wafugaji wamelishia ng’ombe zao katika shamba langu, nakuomba Mkuu wa Mkoa unisaidie nipate haki yangu…. amesema Bi. Juliana.
Naye, Samweli Joseph mkazi wa kijiji cha Mvumi, amesema wafugaji hao wamelishia ng’ombe shamba lenye zaidi ya Ekari mbili lililokuwa na mazao yenye thamani ya shilingi 2,800,000/= kwa mujibu wa Mtathmini huku wao wakitaka kumlipa Shilingi 200,000/=.pekee.
Wito umetolewa kwa wananchi wote Mkoani humo kutojihusisha na vitendo vyovyote vya kihalifu na kuwataka kudumisha Amani, upendo na umoja katika maeneo yao kwa lengo kuimarisha utulivu na kushiriki kwenye shughuli za kujiletea maendeleo yao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.