Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kulitumia vyema gari jipya katika kuyafikia maeneo yote ya miradi ya maji ambayo hapo awali yalikuwa hayafikiki kutokana na upungufu wa magari katika mamlaka hiyo ya Wilaya ya Malinyi.
Mhe. Malima amebainisha hayo Oktoba 24, Mwaka huu wakati wa tukio la kukabidhi gari jipya kwa RUWASA lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Adam amesema lengo kubwa la kukabidhi gari hilo Wilayani humo ni kutokana na upungufu wa magari kwa RUWASA kushindwa kufika kukagua miradi ya maji inayotekelezwa Wilayani humo, hivyo ameitaka mamlaka hiyo kwenda kufanya kazi kwa bidii na kulitumia gari hilo kwa lengo kuwaondolea wananchi adha ya maji.
".. watu wa idara ya maji, Mkurugenzi na viongozi wengine mkalitendee haki kwa matumizi ya gari hili kuweza kuifikia miradi na maeneo yote ya Malinyi na kutatua changamoto za maji..." Amesisitiza Mhe. Adam Malima
Pia Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwatazama Wananchi wa Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro kwa kuwaletea gari kwa ajili ya RUWASA ili kuwatumikia wananchi hasa kutatua changamoto za maji.
Kwa upande wake, Mhandisi Sospeter Lutonja Meneja wa RUWASA wa Mkoa wa Morogoro amesema kupitia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mkoa huo umeendelea kupokea fedha za miradi ya maji ambapo kwa sasa miradi 64 inaendelea yenye thamani ya shilingi Bilioni 89.
Ameendelea kwa kusema moja ya changamoto wanayoipata watendaji wa RUWASA waliopo ngazi za Wilaya ni upungufu wa magari ambapo inawapelekea kushindwa kufika katika miradi ya maji hivyo amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwaona Wananchi wa Malinyi na kuweza kutoa gari ambapo itaenda kuondoa changamoto za maji kwa wananchi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.