Mkurugenzi wa fedha na utawala CPA Prisilla Mushi amewasisitiza watendaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kuwa wabunifu katika kazi zao kwani amesema kumekuwa na mashirika mengi ya ukopeshaji na utoaji huduma za fedha ikiwemo VIKOBA, na kuwataka kuwa na utendaji unaolenga viwango vya kimataifa ili kuwa na mwendelezo mzuri kwa wateja wao na kuongeza wateja zaidi.
CPA Mushi ametoa kauli hiyo Novemba 21, 2023 katika mafunzo ya watendaji wa SACCOS kuhusu masuala ya uhasibu na ukaguzi yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Nashera iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao.
”... sasa hivi taasisi nyingi zinapambana kupata deposit kama vikoba naona mnakuja juu sana kwa hiyo SACCOS mnatakiwa kuwa wabunifu katika utendaji ili kuendana na viwango vya kimataifa...”
Katika hatua nyingine, CPA Mushi amewataka watendaji hao kufuata utaratibu katika kuchukua hati ili kuwa na hati safi ambapo amebainisha kuwa mwaka 2022 hati safi zilikuwa 23% na mwaka 2023 zimekuwa 28.2% huku akibainisha kuwa hati hizo haziridhishi ambapo changamoto kubwa ikiwa kutofuata utaratibu mzuri na kupata hati safi, hivyo mafunzo hayo yatakuwa mwarobaini wa kutibu tatizo hilo.
Kwa upande wake, Kaimu meneja kitengo cha ushauri COASCO CPA. Gabriel Msuya amesema kuwa kitengo hicho kimefanya utafiti na kugundua kuwa baadhi ya watendaji wanakwama kutokana na tatizo la uelewa hasa kwenye kufuata taratibu, kanuni na sheria zote za kupata hati safi, hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha watendaji hao kupata uelewa wa pamoja ili kuondoa changamoto hiyo.
Naye Mshiriki wa mafunzo hayo wa URA SACCOS LTD kutoka Dar es salaam kwa niaba ya washiriki wote amesema kumekuwa na changamoto kubwa katika Vyama vya Ushirika hasa katika hesabu zinazoendana na viwango vya kimataifa hivyo mafunzo hayo anaamini yataboresha utendaji wao wa kazi
Mwisho
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.