Maonesho ya Kilimo Biashara na Mikutano ya Wakulima na Wafugaji (SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2024) yamelenga kuleta mageuzi katika sekta ya Kilimo, ufugaji na mazingira ili kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo na mifugo.
Hayo yamebainishwa Septemba 15, Mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akiongea na waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake kuhusu Maonesho ya Kilimo Biashara yanayoitwa “SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2024, MSIMU WA 3” yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Gairo kuanzia Oktoba 6 - 12, 2024 yakiwa na lengo la kuwasaidia wakulima na wafugaji kupata huduma na kujifunza teknolojia na mbinu bora za uzalishaji.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amesema maonesho hayo pia yamelenga kutekeleza maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na ufugaji kupitia mkakati wa Ajenda 10/30 ambao unalenga kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kufika 10% ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia 4.2% Mwaka 2023.
“…tunatakiwa kulima kiteknolojia kwa kutumia nguvu na mtaji kidogo kupata kipato kikubwa ili kupata chakula cha ziada na kuweza kuondoa umasikini…” amesema Mhe. Adam Kighoma Malima
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema dira na mikakati ya Mkoa kwa Wilaya ya Gairo, ni kuwasaidia wananchi kulima na kufuga kwa tija kupitia mazao ya asili yanayolimwa Wilayani humo sambamba na mazao mbadala ya kimkakati kama parachichi, viazi mviringo na tumbaku, ikiwa ni nyenzo muhimu ya kukuza vipato vya wananchi wa Wilaya hiyo.
Kwa muktadha huo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kuendelea kujikita katika kilimo mazao, kilimo uvuvi na kilimo mifugo sambamba na utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi, umeme, mkaa mweupe na njia nyingine mbadala ili kutunza vyanzo vya maji ambavyo vinachochea kupata mazao bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame amesema, zaidi ya asilimia 95 ya wananchi wa Wilaya hiyo wanajishughulisha na sekta ya kilimo pamoja na mifugo hivyo maonesho hayo ya Kilimo biashara ni muhimu katika kutoa mafunzo ya kutumia teknolojia ya kilimo kwa uzalishaji wenye tija.
Kwa sababu hiyo, Mhe. Makame amesema Wilaya hiyo imeamua kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta ya kilimo na mifugo ikiwemo tija ndogo na kufanya maonesho ili kuwakutanisha wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo, mifugo na mazingira.
Amebainisha wadau wanaohitajika kukutana katika msimu huu wa tatu wa maonesho hayo kuwa ni pamoja na waukima na wafugaji, wauzaji na wazalishaji wa pembejeo za kilimo na mifugo, taasisi za fedha kwa ajili ya kutoa fursa ya upatikanaji wa mitaji ya masharti nafuu ya kuwekeza katika sekta ya kilimo, mifugo na mazingira.
Wadau wengine amewataja kuwa ni taasisi za utafiti katika sekta ya kilimo na mifugo, wasindikaji na wafanyabiashara katika sekta ya kilimo na mifugo, mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na shughuli za kilimo, mifugo na mazingira, taasisi za umma na binafsi zinazotoa huduma ambatano kwa wakulima na wafugaji ikiwemo taasisi za Bima, hifadhi ya jamii na nishati safi ya kupikia.
Dhamira kubwa hapa ni kutekeleza maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhifadhi mazingira hapa nchini, kuondoa umasikini kwa watanzania, kukuza uchumi wao na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa na watu wake.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.