Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewataka Wananchi kutoka vijiji vinavyopakana na Pori Tengefu la Mto Kilombero pamoja na Hifadhi za taifa zilizo karibu na pori hilo kuacha mara moja tabia ya kusema uongo dhidi ya viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA ambao wanalinda eneo hilo badala yake wawe wa kweli katika kutoa kero zao kwa Serikali
Loata Sanare ametoa kauli hiyo Novemba 27 mwaka huu alipokutana na wawakilishi wa wananchi kutoka vijiji 43 vya Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero wakiwemo Wenyeviti wa vijiji na Viongozi wengine wa Serikali kikao ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mlimba katika Mji mdogo wa Ifakara ili kujadili kero mbalimbali zinazojitokeza baina ya wananchi na Taasisi za Serikali za TAWA na TANAPA.
Amesema pamoja na kuwa walinzi wa kwanza katika Pori Tengefu na Hifadhi za Taifa ni wananchi wenyewe lakini bado Serikali imekasimisha jukumu la kulinda maeneo hayo kwa TAWA na TANAPA ambapo ni wajibu wao kutembelea maeneo hayo na kulinda, lakini baadhi ya wananchi wameonekana kuwazuishia uongo mara kwa mara Maofisa wa TAWA na TANAPA na kuwataka waachane mara moja tabia hiyo.
“Watu wa TAWA wana kosa gani kupita na kuangalia maeneo hayo, sasa wanafanya ukorofi wa kuanza kuwatukana na kuwatungia uongo, sasa hii si sawa. Viongozi tuwatetee wananchi wetu kwa mambo ya kweli yale ambayo si ya kweli hapana, nasema hapana mbele yenu na mbele ya TAWA na TANAPA” alisema Sanare.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa kuwa kuna baadhi ya wananchi katika maeneo hayo ya Pori Tengefu wamekuwa wakitoa taarifa kwa viongozi wa juu wa Serikali na chama taarifa ambazo nyingine ni za uongo na za kufitinisha baina ya wananchi na TAWA au TANAPA jambo ambalo Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kuacha tabia hiyo ili waweze kusaidiwa pale ambapo kweli kuna uonevu dhidi yao.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwakumbusha wananchi kuwa pamoja na Serikali kujali maisha yao lakini Serikali haitakubali eneo la Pori Tengefu na Ardhi Oevu yam to Kilombero kuvamiwa kwa sababu ni chanzo kikubwa cha maji yatakayotumika katika kuendesha Mradi mkubwa wa Umeme wa Mwalimu Nyerere unaoendelea kujengwa ambao utawafaidisha watanzania wengi na sio wa Wilaya hizo tatu pekee.
Kwa upande mwingine Loata Sana amewataka Maofisa wa kutoka TAWA na TANAPA waendelee kutekeleza wajibu wao lakini kwa kufuata taratibu zote za kiserikali ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali ya kijiji pale ambapo wanataka kutekeleza majukumu yao ndani ya kijiji husika.
Mwisho, Mkuu wa Mkoa alihitimisha kikao hicho kwa kuwaagiza wakuu wa Wilaya kuunda Kamati za Uchunguzi wa migogoro na kero zinazotolewa na wananchi na namna nzuri ya kufanya oparesheni ya kutoa mifugo katika pori tengefu, huku akitaka shughuli zote za kibinadamu ndani ya pori hilo kusimama laikini pia Elimu juu ya umuhimu wa pori hilo iendelee kutolewa kwa wananchi.
Kwa upande wao wataalamu wa TAWA akiwemo Laurence Okode ambaye ni Meneja wa Pori Tengefu la Mto Kilombero pamoja na Joseph Chuwa ambaye ni Afisa Maliaasili kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wamesema serikali isipoingilia kati uvamizi unaoendelea sasa katika Pori Tengefu utapelekea Mradi mkubwa wa Ufuaji Umeme wa Mwalimu Nyerere kutokuwa wa ufanisi zaidi huku wakithibitisha kuwa zoezi la kuiweka mipaka inayolalamikiwa na wananchi lilikuwa shirikishi.
Katika mjadala huo wananchi wamelalamikia juu ya mipaka ya mwaka 2012 na 2017 iliyowekwa na TAWA kwa madai kuwa hawakushirikishwa jambo ambalo Maofisa watawa wameeleza kuwa zoezi la hilo lilikuewa shirikishi na mihutasari yake ipo.
Kikao hicho kilichoshirikisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo, Wakuu wa Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi, Wahe. Wabunge, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya hizo, wenyeviti wa vijiji wote kutoka katika Wilaya hizo, Maafisa wa Tarafa, watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji pamoja na Maofisa wa kutoka taasisi za TAWA na TANAPA kililenga kujadili ongezeko la kero mbalimbali kutoka kwa wananchi wanaopakana na maeneo ya Pori Tengefu la Kilombero na hifadhi za wanyama katika maeneo hayo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.