Sekretarieti ya Mkoa yaahidi maji nanenane
Na mwandishi wetu Morogoro
Timu ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro imeahidi kufanya ufuatiliaji wa kina na wa karibu kuhakikisha changamoto sugu ya Maji ambayo hujitokeza kila mwaka katika viwanja vya Nanenane inatafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili kutoathiri vipando wakati wa maonesho ya Nanenane ya kila mwaka.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Mkoa wa Morogoro wakitembelea mabanda ya maonesho. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Ezron Kilamhama
Kauli hiyo imetolewa Agosti 2 mwaka huu na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Miundombinu Mhandisi Ezron Kilamhama ambaye aliongoza Timu ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa huo baada ya walipotembelea na kujiridhisha namana maonesho ya Nanenane 2022 yalivyoandaliwa na yanavyoendelea.
Ni katika kujaribu uzuri wa bidhaa za nanenane, Hapa Katibu Tawala Msaidizi wa Sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Morogoro, Anza Amen Ndossa akijaribu kukalia moja ya makochi yanauzawa katika banda la JKT
Akiongea kwa niaba ya timu hiyo mara baada ya kutembelea mabanda kadhaa ya maonesho hayo, Mhandisi Kilamhama amesema timu imeridhishwa na maandalizi yaliyofanyika kwa muda mfupi akapongeza Kamati ya maandalizi ya Maonesho hayo kanda ya Mashariki inayoundwa na wajumbe kutoka Mikoa minne ya Tanga, Dar es Salaa, Pwani na wenyeji Morogoro.
Wajumbe wa Menejimenti wakifurahishwa na vipando vya mboga mboga
Wajumbe wa Sekretarieti. kulia ni Dr. Rozaria Rwegasira Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro, ndiye mwenyeji wa Shughuli za Nanenane katika Ofisisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
Pamoja na pongezi hizo aligusia channgamoto ya upatikanaji wa Maji ndani ya uwanja huo wa nanenane na kukiri kuwa ni kweli changamoto ya maji imekuwa sugu, kwa sababu hiyo amesema Mkoa ubabeba changamoto hiyo na kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro (MORUWASA) Watahakikisha wanatafuta jawabu la kudumu ili maonesho yajayo yaondokane na adha hiyo.
“.....na tutatoa msukumo wahakikishe kwamba maji yanapatikana katika maeneo haya ili basi mapando haya yawe endelevu yasiwe yanaandaliwa wakati wa maonesho halafu baada ya hapo yanapotea” amesema Mhandisi Kilamhama.
Katika kuridhishwa huko wajumbe wengine walivutiwa na zana za kilimo, yakiwemo matrekta. Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Morogoro Leopold Ngirwa (pichani juu) yeye amevutiwa na ubora wa trekta hilo.
Katika hatua nyingine Kaimu Katibu Tawala huyo amewakumbusha Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Mikoa inayounda kanda ya Mashariki kurejea na kutekeleza agizo la Mgeni rasmi aliyetembelea maonesho hayo Agosti mosi mwaka huu la kuandaa vipando katika Halmashauri zao ili kutoa elimu ya kilimo kwa wananchi ambao hawakupata hawakufika maonesho ya nanenane huku wakikumbuka kuwa kwa sasa kwa wananchi hao Kilimo ni BIASHARA kwao.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2022, yameanza kushamiri tangu Julai 31 mwaka huu na yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Agosti 4 na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyoko Nanenane Mkoani Morogoro.
Kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka huu ni Ajenda ya 10/30, Kilimo ni Biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango Bora ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.