Sekta ya Afya Mkoani Morogoro imeweka mikakati ya kuwawezesha Wauguzi kutafuta mbinu za kupunguza vifo vya Mama na Mtoto vinavyotokana na uzazi kwa kufuata kanuni na taratibu za kuwahudumia wananchi.
Hayo yamebainishwa Mei 24, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa katika maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika Kituo cha Afya cha Sabasaba kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
Dkt. Mussa amesema vifo vya Mama na Mtoto vimepungua kutoka 115 hadi 85 kwa mwaka 2022/2023 kwa kila watu laki moja na kuwataka wauguzi kuendelea na jitihada hizo za kupunguza na ikiwezekana kukomesha kabisa vifo vinavyotokana na uzazi.
"...hadi sasa takwimu zinaonesha mmefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 115 hadi 85 kwa kila watu laki moja kwa mwaka 2022 hadi 2023..." amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa amewataka wauguzi kujiendeleza kielimu kwa kutumia elimu za kimtandao (Online Education) ili kuwa na wakati mzuri wa kuendelea na kazi sambamba Mkoa kutokuwa na uhaba wa wafanyakazi katika vituo vya afya.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala huyo ameishauri sekta ya Afya Mkoani humo kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo mashamba ya miti ya kudumu likiwemo zao la Karafuu na Kokoa na kuahidi kutoa bure eneo kwa ajili ya uwekezaji huo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetumia au kuwekeza Tsh. Bil. 30 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya sekta ya Afya.kwa miaka mitatu mfululizo
Ameongeza kuwa pia Serikali imetenga ama kuwekeza Tsh Bil.10 kwa ajili ya kununuzi wa madawa kwa kipindi cha miaka miwili huku akisisitiza watendaji wa Sekta ya Afya wa Hospitali na Vituo vya afya kusimamia vyema utoaji wa huduma kwa wateja (Customer care) kwa kutumia lugha yenye matumaini.
Nae, Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Morogoro Dkt. Awadhi Juma Utime amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya wauguzi 1737 katika vituo mbalimbali vya Afya huku akibainisha upungufu wa Wauguzi 4297 na kuiomba Serikali kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo ya upungufu wa Wauguzi.
Maadhimisho hayo ya wauguzi duniani yamefanyika Mkoani Morogoro yakiwa na kaulimbiu isemayo "Wauguzi sauti inayoongoza wekeza katika uuguzi, heshimu haki na Linda haki".
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.