Zoezi la sensa ya majaribio ya watu na Makazi katika Mkoa wa Morogoro limefanyika na kufanikiwa kwa zaidi ya asilimia 100 baada ya kaya zilizokusudiwa kuhesabiwa kuzidi matarajio ya wajumbe wa kamati ya sensa ya Mkoa huo.
Hayo yamebainishwa Septemba 16 mwaka huu na Mratibu wa Sensa wa Mkoa huo Charles Mtabo wakati akitoa taarifa ya zoezi hilo kwa Kamati ya Sensa ya majaribio ya Mkoa ilipotembelea eneo la zoezi Mtaa wa Mtawala katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya zoezi hilo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja (wa pili kulia) akiwa na wajumbe wa kamati ya sensa ya majaribio Mkoa wa Morogoro katika Mtaa wa Mtawala Kata ya Mwembesongo.
Akifafanua zaidi, Mtabo amesema jumla ya kaya 332 za Mtaa huo zimehesabiwa kwenye zoezi hilo hivyo kuvuka lengo la kaya 300 zilizokuwa zimelengwa kuhesabiwa katika Mtaa huo uliopo kata ya Mwembesongo.
Katika hatua nyingine, Mtabo amebainisha kazi mbalimbali zinazofanyika katika sensa hiyo ya majaribio kuwa ni pamoja na kutambua mipaka ya kuhesabu watu, kuendesha sensa ya watu na makazi kwa wakazi wote waliolala usiku wa kuamkia siku ya sensa na kuendesha zoezi la kupata Anuani za makazi.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya Sensa ya Mkoa amesema kufanikiwa kwa zoezi hilo kwa zaidi ya asilimia 100 ya kaya zilizohesabiwa zinatokana na hamasa iliyofanyika katika kutoa Elimu kwa wananchi wa mtaa huo juu ya umuhimu wa zoezi la sensa ya majaribio.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja (kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro.
Aidha, amewapongeza wananchi wa mtaa wa Mtawala na kuwataka kuwa mabalozi wakati wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 27 kuamkia 28, 2022 ili kuisaidia Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupanga bajeti nzuri itakayokidhi huduma zote za kijamii kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
‘’Bila uhamasishaji zoezi hili halitofanikiwa, kwa hiyo sisi tunajipanga kufanya uhamasishaji wa nguvu kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa huu’’ amesema Mtunguja.
Kwa upande wake Mshauri wa Bodi ya Wajumbe wa Sensa Dkt. Nicolaus Shombe, ameeleza kuwa sensa ya mwaka huu ni tofauti na nyingine zilizopita kutokana na zoezi hilo kuhusisha wajumbe wa zoezi hilo kutoka eneo husika.
‘’Kama labda unaenda sehemu ambayo ni jamii ya wafugaji watatumika watu wa jamii hiyo, kwa hiyo hata tukienda kwenye makundi ya watu maalum watatumika watu hao ili kuondoa dhana potofu walionayo baadhi ya watu katika zoezi hili’’ amesema Shombe.
Naye Msimamizi wa Sensa Kanda ya Pwani na Morogoro Dkt. Joyce Peter amebainisha umuhimu wa kutambua Anuani za makazi katika jaribio hilo kuwa ni kusaidia kutambua sehemu anapoishi mtu kwa urahisi ili kufikisha taarifa ama huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
Akizunguzia namna ambavyo zoezi hilo liaendelea kufanyika Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwembesongo Amina Said ambaye pia ni Katibu wa Sensa ngazi ya kata hiyo, amesema zoezi hilo limefanyika kwa ufanisi na watahakikisha changamoto chache zilizojitokeza wanakabiliana nazo ili mwakani zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi zaidi.
Sensa ya watu na Makazi hapa nchini inatarajiwa kufanyika mwakani agosti 27 kuamkia 28 ambapo mwaka huu serikali imeteua mikoa 13 hapa nchini kwa ajili ya kufanya sense ya majaribio ya watu na makazi ukiwemo Mkoa wa Morogoro katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kata ya Mwembesongo Mtaa wa Mtawala.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.