Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuboresha sekta ya madini hivyo, wachimbaji wadogo wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta hiyo na kuzingatia tafiti za uchimbaji madini kulingana na mabadiliko ya kisayansi yaliyopo kwenye sekta hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima Novemba 13, 2024 wakati akifungua mkutano wa wadau wa madini Mkoa wa Morogoro uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Uluguru katika Manispaa hiyo ukiwa na lengo la kuhamasisha shughuli za uchimbaji wa madini ndani ya Mkoa huo.
Kwa sababu hiyo amewataka wachimbaji wadogo kutumia fursa ya kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita kuchangamkia fursa hiyo ya sekta ya madini kujiunga pamoja, kuchukua mikopo banki na kuendeleza shughuli zao za uchimbaji.
".. Bado nawahimiza msiache mbachao kwa msala upitao, fursa iliyopo kwa sasa hivi kwa maendeleo ya sekta yenu ni kubwa sana nakuombeni muitumie.." amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Aidha Mhe. Malima amekemea tabia ya baadhi ya wachimbaji wa madini kuchimba kwa kutozingatia taratibu na kanuni jambo ambalo hupelekea uharibifu wa vyanzo vya maji na kusababisha madhara kwa watumiaji wa maji kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Mhe. Adam Malima amewaahidi wachimbaji wa madini mkoani humo kuwapa ushirikiano wa kutosha hususan wakati wanapopata changamoto zikiwemo changamotoza za mikopo kwa lengo la kuwaendeleza na kuwainua kwa maslahi mapana ya Taifa.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima amefurahishwa na ongezeko la wachimbaji wa madini wakike na kuwapongeza wachimbaji hao kwa kujitoa kufanya kazi hizo ambazo huwapatia kipato chao na kuongeza pato la Mkoa.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro Bi. Zabibu Napacho amesema katika Mkoa wa Morogoro kuna jumla ya leseni za uchimbaji wa madini 2413 ambapo leseni 205 zinafanya kazi na leseni 2208 hazifanyi kazi, aidha Mkoa una jumla ya leseni za tafiti za madini 61 ambapo 18 zinafanya kazi na 43 hazifanyi kazi.
Pia kiongozi huyo ameiomba Mamlaka zinazo shughulikia maji, Barabara na Umeme kuboresha miundombinu katika maeneo ya migodi ili kuweza kufanya kazi mbalimbali zikiwemo za usafiri na usafirishaji kwa urahisi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Morogoro (MOREMA) Dr. Mzeru Omari ameeleza changamoto wanazokutana nazo wachimbaji wadogo kuwa ni pomoja na ukosefu wa soko kwa ajili ya kufanya biashara ya madini huku akiiomba Serikali kuwapatia vifaa vya kisasa vya upimaji na utambuzi wa madini chini ya ardhi ili kuondokana na uchimbaji wa madini wa kubahatisha.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.