Serikali inapoteza zaidi ya Shilingi Mil.52 kila siku sawa na zaidi ya Bil.18 kwa mwaka kutokana na magari yanayopita katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi bila kulipa tozo.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Afisa Mhifadhi daraja la pili Mikumi Samwel Mguhachi wakati wa kikao cha kukuza na kuendeleza utalii na vivutio vingine Mkoani Morogoro kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Mguhachi amebainisha kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2018 zaidi ya magari 2,218 yanapita hifadhini kwa siku na kuangalia vivutio bila kulipia tozo zozote ambapo mbali na magari hayo yaliyo kwenye safari pia baadhi ya waongoza wageni wamekuwa wakitumia fursa hiyo kufanya utalii bure.
Kutokana na upotevu wa mapato hayo, Mguhachi ameiomba Serikali kuanzisha tozo ya magari yanayopita katika barabara ya TANZAM kama ilivyo katika barabara zilizo katika hifadhi nyingine kwa kuwa hii pia ni fursa ya kuongeza mapato kwa Serikali.
Sambamba na ombi hilo, Mguhachi ameiomba Serikali kuweka utaratibu mahususi wa kupunguza au kuzuia kabisa upitaji wa magari nyakati za usiku kwenye barabara kuu inayopita katikati ya Hifadhi kwani ndio muda pekee ambao kumekuwa na matukio mengi ya wanyama kugongwa na matukio mengine ya uhalifu.
Akibainisha changamoto zilizopo katika sekta ya utalii Mkoani Morogoro Afisa Wanyamapori wa Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa amesema kuna uwekezaji mdogo katika utalii hususan katika makampuni ya kusafirisha watalii.
Pia, Chuwa amebainisha changamoto nyingine kuwa ni ubovu wa miundombinu, kutotangazwa vivutio vya utalii, uharibifu wa mazingira unaotishia uhai wa vivutio vilivyokuwepo na upungufu wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiutalii.
Akitoa taarifa ya hali ya vivutio vya utalii katika Mkoa huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema, Mkoa huo kwa sasa umejipanga vizuri kuwa wa Kiutalii kwa kutambua vivutio vyote vilivyopo katika Halmashauri tisa za Mkoa huo na kuandaa mwongozo ambao utahusisha mbuga za wanyama na utamaduni yaani vivutio vya asili.
Sambamba na hayo, Mhandisi Kalobelo ametoa wito kwa wadau wa kikao hicho kufikiria namna Mkoa wa Morogoro unavyoweza kujikuza kitalii kutokana na vyanzo vingi vya kitalii vilivyopo katika Mkoa huo hali itakayopelekea kuinua uchumi wa wananchi wake, Mkoa na Taifa kwa kwa ujumla.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho amesema lengo kubwa la kikao hicho ni kuweka uelewa wa pamoja wa vivutio vilivyopo katika Mkoa huo, kutambua changamoto na kuweka mikakati ya kuendeleza utalii katika Mkoa na taifa kwa ujumla.
Pia, Loata Sanare amebainisha kuwa hadi sasa sekta ya utalii inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la taifa na kiasi kidogo ukilinganisha na utajiri wa vivutio na rasilimali nyingine zilizopo katika Mkoa wa Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.