Imeelezwa kuwa Serikali itaendelea kutafuta njia za kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyote vya Afya vilivyopo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa Machi 27 mwaka huu na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Tawala na Rasilimali Watu Bw. Herman Tesha wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa Shitiri yaliyofanyika katika Hoteli ya Glonency iliyopo Katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Katibu Tawala huyo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na dawa unafikia asilimia 100 katika vituo vyote kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Mikoa hapa nchini, hivyo umeanzisha mfumo huo wa mshitiri kwa lengo la kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unafikia asilimia 100 na kuondoa changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya.
Amesema kupitia mfumo huo wa Mshitiri ambao Serikali imeuanzisha, utasaidia kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na dawa kutoka kwa mashirika binafsi yanayotambulika na Serikali ili kuifikia asilimia 100 inayotakiwa baada ya MSD kushindwa kufikia asilimia hizo.
Aidha, Bw. Tesha amewataka watendaji wa Halmashauri kusimamia ukusanyaji wa mapato katika vituo vya afya ili kufikia lengo la asilimia 100 kwa kuwa mapato hayo ndiyo yatakayo fanikisha upatikanaji wa vifaa tiba hivyo pamoja na dawa.
Kwa upande wake mwezeshaji wa Kitaifa wa mfumo huo Dkt. Abdilah Njopeka amesema lengo la mafunzo hayo ni kutawanya mwongozo wa utekelezaji wa mfumo huo ili kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa dawa.
Nae Bi. Fiona Chilunda Mshauri Mwandamizi wa masuala ya dawa na vifaa tiba kutoka mradi wa HPSS amesema wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa asilimia 100, ameongeza kuwa mfumo huo utafanya kazi pale ambapo MSD ikishindwa kutekeleza mahitaji ya vituo vya afya kwa asilimia hizo 100.
Dkt. Mariam Bendera akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro ameishukuru Serikali kwa kuwaletea mafunzo ya mfumo huo ambao utawasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji na uendeshaji wa vituo vya afya kwa kuwa hali ya upatikanaji wa vifaa tiba na dawa utaimarika Zaidi kupitia mfumo huo.
Lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha utekelezaji wa Mfumo huo wa Mshitiri ambao ulizinduliwa Dodoma hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.