Serikali Mkoani Morogoro imesema itaendelea kushirikiana na Vijana kwa kutoa fursa za mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi mbalimbali vikiwemo vikundi vya wajasiliamali, watu wenye ulemavu na wabunifu ili kujikwamua na hali duni ya maisha.
Kauli hiyo imebainishwa Disemba 5, 2024 na Afisa Maendeleo ya vijana Mkoa wa Morogoro Bi. Mariana Lutananurwa wakati akifungua Kongamano la siku moja la vijana lililojumuisha vijana kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Uingereza, Uganda na Tanzania lililofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo kikuu cha Jordan mjini Morogoro .
Akifungua kongamano hilo lililolenga kuwakutanisha vijana wanaojitolea katika sekta binafsi na sekta za umma ili kutoa elimu, kupeana uzoefu na kujaddili mikakati ya namna vijana kushiriki kwenye maendeleo endelevu, Bi. Mariam Lutananurwa ametumia fursa hiyo kuwaahidi vijana hao kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu itaendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kupitia Halmashauri zake.
Kwa sababu hiyo Bi. Mariana amesema pamoja na shughuli za kujikwamua kimaisha bado Vijana wanao wajibu wa kujikwamua na umaskini huo kwa kuwajibika kuimarisha amani, mshikamano na kutunza maadili ya Taifa.
"....kama vijana tunaowajibu wa kujikwamua na umaskini kwa kuwajibika kuimarisha amani, upendo na mshikamano..." amesema Bi. Mariana Lutananurwa.
Akizungumzia shirika la Kijana Initiative Organisation (KIO) ambalo limeratibu kongamano hilo Bi. Mariana amesema shirika hilo limekuja na mpango mkakati wa kuhakikisha vijana wanajikwamua kiuchumi kwa kutoa elimu kupitia wawezeshaji wanaofanya kazi sehemu mbalimbali duniani hivyo amewataka vijana watumie vema fursa hiyo.
Aidha, Bi. Mariana amesema shirika hilo linajihusisha kusaidia vijana hususan wajasiriamali kwa kuwajengea uwezo, kutoa fursa za elimu kwa vijana (scholarship), elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hasa utunzaji wa mazingira na elimu kuhusu matumizi ya mitandao bila kuathiri tamaduni, mila na desturi.
Kupitia shirika la KIO, amesema vijana wataweza kupaza sauti katika kukataa viashiria vya ukatili wa kijinsia, biashara haramu zinaazotokana na mabadiliko ya teknolojia ambayo inaharibu mila na desturi zilizopo huku akiahidi kuwa Mkoa huo utatoa ushirikiano kwa shirika la KIO na kuhakikisha vijana wananufaika na maarifa yatakayotolewa na shirika hilo.
Klwa upande wake, Mkurugenzi wa KIO Bi. Rose Mmbaga amesema shirika hilo limelenga kuwaunganiasha vijana, kuwapa taarifa na kuwahamasisha ili kuweza kuchangia maendeleo endelevu katika jamii na kwamba litawasaidia vijana kupata mawazo mapya kupitia majadiliano na kuweza kuibua changamoto zinazowakabili na kuzitafutia majibu.
Naye, Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo kikuu cha Jordan Bw. Alimia Libela amewashauri vijana kuwa na mitazamo ya kugundua fursa yenye tija ili kuendelea kuisaidia jamii inayowazunguka na kuepuka kuilalamikia serikali kuhusu ajira.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.