Serikali kuendeleza vita dhidi ya UKIMWI.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela amesema Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendeleza mapambano dhidi ya maambukizi ya Virus vya UKIMWI na magonjwa mengine ya mlipuko kwa kushirikiana na wadau mbalimbali lengo likiwa ni kupunguza ama kutokomeza kabisa maambukizi ya magonjwa hayo.
Shigela ameyasema hayo Disemba Mosi mwaka huu wakati wa Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo huadhimishwa Disemba Mosi kila mwaka ambapo mwaka huu Kimkoa yamefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kata ya Mazimbu katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Shigela amesema kuwa, katika kuendeleza mapambano hayo, Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu ya sekta ya Afya kwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kusaidia vita dhidi ya UKIMWI na magonjwa mengine kwa kuboresha huduma za afya ili ndugu zetu walioathirika na ugonjwa huo waweze kupata dawa bila malipo ili kupunguza makali ya virusi hivyo.
Aidha, amesema Serikali imeendelea na jitihada za utoaji wa elimu kwa jamii kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi hayo na pia jamii kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kwa lengo la kujua mwenendo wa afya zao.
“…..Serikali inaendelea kutoa huduma bure za matibatu dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, yote hayo ni mikakati ya serikali ya kuonesha dhamira iliyo nayo, na hasa hasa serikali ya awamu ya sita imekuja na kasi Zaidi ya kuhakikisha mapambano dhidi ya Ukimwi yanaendelea”.
Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa, serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua ama kutokomezwa kabisa hadi kufikia asilimia sifuri huku akiwataka watanzania kuendelea kuchukua taadhari dhidi ya mlipuko wa UVIKO 19 kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando amesema kuwa maambukizi ya VIRUS vya ugonjwa wa UKIMWI kwa sasa yameongezeka hadi asilimia 4.2 kutokana na wimbi la ongezeko la vijana kunzia umri wa miaka 15 na kuendelea, hivyo serikali ya Mkoa imeelekeza nguvu zake katika kuhakikisha kuwa maambukizi yanapungua kwa kutoa elimu kwa jamii kuchukua taadhari na kutoa huduma kwa waathirika wa UKMWI.
Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio, pamoja na kuzungumzia ugonjwa wa UKIMWI kuwa ndani ya kipindi cha miaka 17 maambukizi Mkoani humo yameongezeka kwa asilimia 4.2, amezungumzia hali ya ugonjwa wa UVIKO 19 kuwa mpaka sasa ni watu elfu 46 pekee kwa awamu ya kwanza ndio waliojitokeza kupata chanjo ya ugonjwa huo, hivyo kutoa wito wananchi kuendelee kujitokeza kupata chanjo.
Nae shuhuda wa watu wanoishi na virusi vya UKIMWI Bi. Anna William ambae pia ni makamu mwenyekiti wa Baraza la Konga, ametoa ushuhuda mbele ya Mkuu wa Mkoa kupata maambukizi hayo tangu mwaka 2005 hadi sasa hajatetereka kimaisha kwa kuwa mara alipojigundua ana maambukizi hayo alianza kutumia dawa za ARV, hivyo amewataka watanzania kwenda kupima afya zao mara kwa mara, na kuepuka ngono nzembe ili kupunguza maambukizi hayo.
Maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI duniani kwa mwaka huu yana kauli mbiu isemayo ”Zingatia Usawa, Tokomeza UKIMWI, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.