Serikali hapa nchini imesema inaweka mipango na mikakati ya kusimamia upatikanaji wa umeme wa kutosha katika maeneo ya Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ili kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kuja kuwekeza na kujenga viwanda mbalimbali kwa maendeleo ya watanzania.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amebainisha hayo leo Agosti 5, 2024 wakati wa Mkutano wa hadhara katika Mji mdogo wa Ifakara na kuongea na wananchi wa Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero katika viwanja vya CCM vilivyopo Mjini Ifakara.
Dkt. Samia amesema ili kuongeza thamani ya viwanda hapa nchini ni lazima nishati ya umeme iwepo ya kutosha ili kuvutia wawekezaji kuja kwa wingi kujenga viwanda na kuongeza thamani ya mazao kwa maendeleo ya Wilaya hizo na Taifa kwa ujumla.
"... Niwahakikishie kwamba Serikali itasimamia kuwa na umeme wa uhakika katika maeneo haya na kufanya uwekezaji uwe mkubwa zaidi na kuleta maendeleo kwa watu wa Kilombero, Ulanga na Malinyi.." amesisitiza Dkt. Samia .
Aidha Dkt. Samia amesema kupitia Wakala wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) wameweza kusambaza umeme kwa vijiji 110 vya Wilaya ya Kilombero na kazi iliyobaki ni kusambaza nishati hiyo kwenye vitongoji na kuunganisha kwenye taasisi na kwa wananchi.
Aidha Dkt. Samia amesema, Serikali inatumia gharama kubwa kujenga miundombinu ya Elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa pamoja na shule za ufundi ili kuwawekea mazingira mazuri vijana wapate elimu, hivyo ametoa wito kwa wazazi hapa nchini kuwapeleka watoto shule kwa lengo la kupata maarifa na ujuzi utakao wasaidia katika kujiajiri na kuajiriwa katika viwanda mbalimbali.
Katika hatua nyingine Dkt. Samia ameagiza viongozi wa Serikali ngazi ya wilaya na Mkoa wa Morogoro kusimamia wakulima wa zao la mpunga wauze kwa bei ya faida ili kukuza uchumi wao badala ya kuuza mazao yao kwa hasara ikiwemo kuuza mpunga kwa kutumia mfumo wa lumbesa jambo ambalo amelikemea.
Sanjari na hayo Dkt. Samia amesema Serikali inampango wa kulifanya bonde la Kilombero kuwa bonde la umwagiliaji ambapo wataanza ujenzi wa mabwawa ya kuhifadhia maji yanayoingia kwenye bonde hilo, maji hayo yataifadhiwa wakati wa mvua na wakati wa kiangazi wakulima watayatumia kwa ajili ya umwagiliaji, hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano ili kukamilisha mradi huo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.