SERIKALI KUJENGA BARABARA YA LUPILO – MALINYI KWA KIWANGO CHA LAMI, Bil. 18 ZATOLEWA KUJENGA MADARAJA MAWILI.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko mbioni kujenga barabara ya Lupiro hadi Malinyi kwa kiwango cha lami ili kuwaondole adha wananchi wa Wilaya ya Ulanga na Malinyi ambao hukumbana na changamoto hizo kila mwaka katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Kauli hiyo ya serikali imebainishwa Aprili, 24, 2025 na Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega alipotembelea Wilaya za Kilombero na Malinyi Aprili 24, 2025 baada ya kujulishwa uwepo wa uharibifu mkubwa wa madaraja kusombwa na maji na baadhi ya barabara za Wilaya hizo kuharibiwa na Mvua zinazoendelea kunyesha sasa.
Waziri huyo wa Ujenzi aliyeambatana na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Alhaji Adam Kighoma Malima waliwasili katika Wilaya hizo wakitokea Mkoani Dodoma kwa njia ya Helkopta na kutembelea maeneo yaliyoharibiwa.
Akiwa Wilayani Malinyi, Waziri Ulega amewaambia wananchi wa Wilaya hiyo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa shilingi Bil. 18 kwa ajili ya kujenga madaraja mawili, ya Mto Fulua na daraja la mto uliopo Kijiji cha Iragua ambayo ni korofi na huleta adha kwa wananchi wa Wilaya hizo.
“Rais samia ameniambia kwamba haya madaraja yalikatika toka mwaka jana Rais amekupeni pesa shilingi Bilioni 18 hizo ni za madaraja peke yake ”
Aidha, Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha mbele ya wananchi hao kuwa Rais Samia Suluhu Hassan pia ameridhia ujenzi wa Barabara ya kutoka Lupilo Wilayani Ulanga hadi Malinyi kwa kiwango cha lami yenye urefu wa zaidi ya km.100 itakayojengwa kwa bajeti ya mwaka 2025/2026.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Alhaji Adam Kighoma Malima awali alimuomba Waziri wa Ujenzi kupata ufumbuzi wa kudumu wa madaraja ambayo husombwa na maji kila mwaka na kusababisha changamoto ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Wilaya za Malinyi na Ulanga.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.