SERIKALI KUJENGA MADARAJA YA CHAKWALE, NGUYAMI
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema iko katika hatua za mwisho kuanza kujenga madaraja mawili ya Chakwale na Nguyami Wilayani Gairo ili kuwaondolea kero ya muda mrefu wananchi wa maeneo hayo.
Hayo yamebainishwa Februari 22 na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa wakati wa ziara yake ya siku Nne Mkoani Morogoro ya kukagua miundombinu ya Barabara ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtaka Waziri huyo kufika kusiko fikika ili kutatua kero za wananchi hususan miundombinu ya Barabara.
Akiwa Wilayani Gairo amewaambia wananchi kuwa Serikali chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan imekwisha ridhia ujenzi wa madaraja hayo mawili ya Chakwale na Nguyami ambao ujenzi wake unatarajiwa kuanza Juni 2024, Daraja la Chakwale likiwa na urefua wa mita 80 na lile la Nguyami likiwa na urefu wa mita 100, lengo ni kuwaondolea wananchi kero ya kupoteza Maisha wa eneo hilo na mali zao.
Aidha, Waziri Bashungwa amemuagiza Mtendaji wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROAD), kufanya usanifu wa kina wa madaraja hayo ili yawe ya viwango na yaje kutumika pia wakati watakapoamua kujenga Barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Akiwa Wilayani Kilosa Waziri Bashungwa amemtaka mkandarasi anayejenga Barabara ya kutoka Rudewa hadi Kilosa mjini kwa Kiwango cha lami kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha Barabara hiyo ifikapo Aprili 22 mwaka huu kwa kuwa hana kisingizio tena kwani fedha alizokuwa anazidai shilingi Bilioni 4 amekwisha lipwa.
Mbunge wa Jimbo la Gairo Mhe. Ahamed Shabiby ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kujali wananchi katika kuwaletea maendeleo yao kwa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Miundombinu na kuweka bayana kuwa hakuna Serikali iliyotoa fedha nyingi kwa Sekta ya Miundombinu kama Serikali ya awamu ya sita.
Akimkaribisha Waziri Bashungwa kuongea na wananchi wa maeneo ya Chakwale, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Wilaya ya Gairo ndiyo Wilaya maskini kuliko zote Mkoani humo, hata hivyo amesema endapo Barabara za kutoka Gairo Kwenda Kilindi Mkoani Tanga na Barabara ya kutoka Mjini Gairo Kwenda Nongwe zitaboreshwa, Wilaya hiyo ndiyo yenye Uchumi mkubwa kupita Wilaya nyingine.
MWISHO.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya chakwale akiwemo Robert John na Simon John, wameiomba Serikali iwajengee madaraja hayo kwa kuwa yamepoteza Maisha ya watu wengi kuchukuliwa na maji Pamoja na mali zao na kwamba Barabara hiyo ndiyo Barabara inayotumika Kwenda Makao makuu ya Wilaya ya Gairo na Hospitali ya Wilaya hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.