Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (Mb) amesema Serikali imetenga bilioni 15 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kununua magari na pikipiki nchi nzima ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa vyombo vya usafiri kwa Jeshi la Polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (kushoto) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima wakati wakikagua kituo cha Polisi kata ya Mvomero.
Waziri Masauni ameyasema hayo Julai 14 mwaka huu alipotembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha Polisi kat a ya Mvomero ikiwa ni ziara ya siku moja katika Wilaya hiyo Mkoani Morogoro.
" ...Serikali itanunua pikipiki kwa ajili ya vituo vya Polisi vya kata nchi nzima pamoja na magari kila Wilaya, tayari bilioni 15 zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha hilo..."amesema Waziri Masauni.
Wakati akiwa kwenye mkutano na wananchi wa Kata hiyo Waziri Masauni amewataka wananchi kuthamini juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea wananchi wake maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo Sekta za Afya, maji, elimu, umeme na miundombinu ya barabara.
Mhe. Mhandisi Hamad Masauni Waziri wa Mambo ya Ndani akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa eneo la Wami-Dakawa Wilayani Mvomero.
Sambamba na hilo, Mhe. Hamadi Masauni ameahidi kufanyia kazi kero zilizotolewa na wananchi ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wanyonge na kwa wale wanaostahili kupata haki hiyo.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amemshukuru Waziri huyo kwa kuwapatia vitendea kazi jeshi la polisi ikiwemo vyombo vya usafiri ili kuongeza ufanisi wa jeshi hilo katika utendaji wao wa kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza na wananchi wakati wa mkutano.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameahidi kufanya ziara katika Wilaya hiyo kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Hassan Omary amesema suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila raia, hivyo amewataka wananchi kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi katika maeneo yao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Bw. Haruna Ally mkazi wa Wami-Dakawa wakati akitoa kero zinazowasumbua amesema wakulima wa eneo hilo wanasumbuliwa na wafugaji kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima, hivyo ameiomba mamlaka husika kushughulikia suala hilo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.