Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) amesema mwaka huu Serikali imepanga kuuza asali nje ya nchi tani 148,000, hivyo amewataka wafugaji wa nyuki kuzalisha asali hiyo kwa wingi ili kutimiza lengo hilo.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo Agosti 4 mwaka huu alipotembelea banda la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni siku ya nne tangu kufunguliwa kwa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki.
Waziri huyo amesema kwa sasa asali inayouzwa ni 5% tu hivyo Serikali kupitia Wizara hiyo imepanga kuongeza uzalishaji kwa kutoa elimu kwa wafugaji wa nyuki ili waweze kuongeza kiwango cha uzalishaji na kufikia zaidi ya asilimia 50% ya asali inayouzwa nje ya nchi.
“...tunauza asali nje ya nchi kwa 5% ambapo mpango wetu wa Wizara ni kuuza tani 148,000 za asali kwa mwaka huu, maana yake ni kwamba tuzalishe tani 148,000 tuongeze uzalishaji kutoka 5% ikibidi tufikie hadi 50%...” amesema Waziri Mchengerwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea zawadi ya begi kutoka kwa mwakilishi wa kikundi cha wajasiliamali katika banda la Halmashauri ya Kibaha.
Aidha, Mhe. Mchengerwa ameitaka benki ya Azania ambayo inatoa mikopo yenye riba nafuu ya 1% kwa wanawake kutanua wigo wa utoaji wa huduma katika maeneo ambayo hayana matawi ya benki hiyo ili kila mwanamke apate fursa ya mkopo huo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa (aliyevaa kofia) akimsikiliza Bw. Josephat Mruma kwenye banda la Azania benki.
Akitoa shukrani kwa Waziri huyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameahidi kuandaa mazingira mazuri ya kuhifadhia wanyama ambao wamekuwa sehemu ya kivutio kikubwa cha maonesho hayo.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amesema wataweka utaratibu ili maonesho hayo yasiishie kipindi cha Nanenane pekee, hivyo utaratibu huo utawezesha maeneo hayo kuendelea kuwa kivutio.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema Kanda ya Mashariki inatafsiri kwa vitendo maelekezo na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Pichani ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa pamoja na Wahe. Wakuu wa Wilaya za Morogoro na Kinondoni wakiangalia zao la mwani.
Kwa upande wake mwakilishi wa Meneja Benki ya Azania Mkoani Morogoro Bw. Josephat Mruma amesema benki hiyo kwa sasa inatoa mikopo ya 1% kwa wanawake ili waweze kujikita katika uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.
Waziri Mchengerwa ametembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika viwanja hivyo na kujionea teknolojia mbalimbali ikiwa leo ni siku ya nne tangu kufunguliwa kwa maonesho hayo.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira akiburudika pamoja na kikundi cha ngoma kutoka Halmashauri ya Bagamoyo.
Hapa Waziri Mchengerwa akiwa pamoja na wadau mbalimbali wanapata elimu ya zao la jongoo bahari kutoka kwa mtaalam wa Uvuvi wa Halmashauri ya Bagamoyo.
Picha za Matukio mbalimbali wakati Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima, viongozi na wadau wa sekta za kilimo, ufugaji na Uvuvi walipotembelea banda la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.