Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoani Morogoro Frank Mizikunte kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa Ardhi watatu ambao walihamishiwa kikazi Wilayani kilosa ambapo hadi sasa hawajawasili Wilayani humo.
Naibu Waziri Angelina ametoa agizo hilo Julai 12, mwaka huu wakati akifanya mkutano na wananchi wa Tarafa ya Magole kata ya Dumira Mkoani Morogoro ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya siku mbili kwa ajili ya kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi inayowakabili wananchi wa Wilaya hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (kushoto) akizungumza na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula kabla ya kuanza kikao cha kusikiliza na kutatua kero za wananchi Wilayani Kilosa.
Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa maafisa Ardhi hao ambao wanatakiwa kuchukuliwa nidhamu ni Kasese Ntolela kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, William Njiha kutoka Dodoma Jiji na Hassani Rashidi kutoka Chalinze hawakuwahi kufika Wilayani humo miaka Miwili hadi sasa.
“Hawa watumishi wachukuliwe hatua za kinidhamu, hatuwezi kuendelea kuwa watu ambao tunawahesabu wapo Wilaya ya Kilosa halafu kilosa hawapo huku migogoro ni mingi isiyoisha kumbe kuna watumishi ambao hawajaripoti’’ amesema Mabula.
Katika hatua nyingine Dkt. Mabula amesema ni kinyume cha sheria za nchi yetu mwananchi yoyote kumiliki hekali zaidi ya Hamsini bila kuidhinishwa na mkutano mkuu wa kijiji husika ambao ndiyo wenye mamlaka ya kujiridhisha juu ya uhalali wa kukupa eneo la Ardhi zaidi ya hamsini.
Aidha, amezitaka Halmashauri za Mkoa huo kutenga fedha kila mwaka kwaajili ya kupima mipaka ya vijiji ambavyo havijasajiriwa na kuhakikisha kuwa vinapatiwa vyeti vya upimaji huo ili kuondoa changamoto za mipaka ambazo zimekuwa zinajitokeza.
Kwa sababu hiyo, Dkt. Mabula amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja Kuunda kamati itakayohusika na kupima mipaka ya vijiji ambavyo havijasajiriwa na kuisimamia kamati hiyo huku akishirikiana na Wahe. Madiwani wa Halmashauri za Wilaya husika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema Mkoa huo utaunda timu ya wataalam ili kubainisha mipaka kati ya kijiji na kijiji na kuandaa alama za kudumu hivyo kuepusha baadhi ya viongozi wasio waadilifu kuuza Ardhi nje ya mipaka ya kijiji chao.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Madiwani na watendaji kuwasilisha kwa Kamishina wa Ardhi kumbukumbu zinazobainisha wawekazaji katika kila kijiji ambao wanamiliki Ardhi hizo kinyume na utaratibu hawayaendelezi maeneo wanayomiliki ili waweze kuzifanyia kazi kumbukumbu hizo mapema iwezekanavyo.
Naye Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro Frank Mizikunte amesema wataanza zoezi la urasimishaji wa Ardhi ili kuepukana na migogoro ya Ardhi ya mara kwa mara inayojitokeza Mkoani Morogoro.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria katika Mkutano huo akiwemo Dotto Yohana na Meriyan Mkunda wamesema mabaraza ya kata ya Ardhi ndiyo visababishi vya migogoro hiyo na kuiomba Serikali kuwapatia kitabu cha sheria za Ardhi wenyeviti wa vijiji ili kuondoa adha ya kuuziwa eneo moja mara mbili.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.