Serikali Mkoani Morogoro imewasilisha rasmi kwa wananchi wa Chanzuru Wilayani Kilosa mkoani humo maagizo ya Serikali yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu kumpatia Bw .Miyanga Laizer shamba la Chanzuru lenye ukubwa wa ekari 1,598 kama mmiliki halali wa shamba hilo ikiwa ni utekelezaji wa Kiongozi huyo wa maagizo aliyoyatoa Novemba 30 mwaka huu Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Taarifa hiyo imewasilishwa Disemba 4 mwaka huu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emannuel Kalobelo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Loata Ole Sanare ambaye hakuwepo katika tukio hilo kwasababu ya majukumu mengine ya kikazi.
Akiwasilisha maagizo hayo Mhandsisi kalobelo amesema pamoja na kuwa shamba hilo kwa muda mrefu limekuwa lina mgogoro huku watu mbalimbali wakiuziana shamba hilo na baadae wananchi nao kuwa na matumizi na shamba hilo, na baada ya uchunguzi wa kina Serikali imeamua kumpa Bw. Laizer kwa sababu ya kuwa mmiliki halali na kuonesha dhamira ya kutaka kuliendeleza kwa kulima zao la Mkonge.
Pamoja na sababu hiyo, bado taarifa hiyo iliyotolewa na Mhe. Waziri Mkuu imeeleza kuwa wananchi ambao tayari wako ndani ya shamba hilo kamwe hawataondolewa bali wataendelea kubaki katika makazi yao na kufanya shughuli nyingine walizokuwa wakizifanya awali na Bw.Laizer atapewa fidia ya maeneo hayo kwa kupewa ardhi nyingine nje ya shamba hilo ili kufidia maeneo ambayo tayari kuna makazi ya watu na mashamba ya wanachanzuru.
“sentensi ya pili. Ardhi ndani ya shamba iliyotumiwa na wananchi itambuliwe na wasiondolewe ili kuepusha kusababisha mgogoro mwingine” ilieleza taarifa hiyo
Aidha, taarifa hiyo iliyosomwa kwa umakini mkubwa na Mhandisi Kaloelo kwa lengo la kutaka kufikisha ujumbe wa Serikali, ilieleza kuwa wananchi waliopata maeneo ya kilimo pamoja na Bw. Laizer mwenyewe wanatakiwa kutumia Ardhi hiyo kwa kulima zao la Mkonge.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi aliwaeleza wananchi kuwa Serikali imefikia hatua hiyo ya maamuzi baada ya kufanya uchunguzi wa kina wa shamba hilo ikiwa ni pamoja na kuwa na vikao mbalimbali ambavyo vyote vilikusudia kutatua mgogoro wa shamba hilo la Chanzuru.
Serikali ya awamu ya tano imefikia hatua hiyo kwa sababu ya sera yake ya kuwajali wananchi hususan wanyonge huku mwenyekiti wa kijiji cha Chanzuru Hassan Nengula kwa niaba ya wananchi ameyapokea maagizo hayo ya serikali huku akibainisha kuwa wanayapokea maagizo hayo hasa kama yatafanyiwa kazi kama yalivyosomwa.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.