SERIKALI MKOANI MOROGORO YAJA NA MRADI WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Shirika la HELVETAS imefanya uzinduzi wa mradi wa Uwezeshaji jamii katika usimamizi endelevu wa misitu (USEMINI) ambapo itasaidia kutunza mazingira kwa kurudisha uoto wa asili na kusaidia kupunguza hewa ukaa.
Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima Aprili 30, 2024 katika hoteli ya Morogoro na na kuhusisha viongozi mbalimbali wa kiserikali na sekta binafsi lengo na kushirikiana katika kutunza mazingira na hivyo kupunguza madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.
Mhe. Malima amesema kupitia mradi huo utasaidia katika kutunza mazingira na kuondoa hewa ukaa pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu upandaji wa miti ya karafuu, kakao, michikichi, kahawa na parachichi ambayo pamoja na kuwa miti hiyo ni rafiki kwa mazingira, watu na maji bado itawasaidia wananchi kuongeza kipato chao.
“… kwa hiyo kampeni yetu ya Mkoa wa Morogoro ni kupanda miche milioni moja moja ya mazao hayo mbadala kwa ajili ya kurudisha uoto wa miti kwa maeneo ambayo yameharibika kwa kukata miti holela kwa ajili ya mkaa na kilimo….” Amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuna umuhimu mkubwa wa wananchi kupatiwa elimu juu ya matumizi ya nishati mbadala hasa matumizi ya mkaa na kuachana na matumizi ya kuni ambayo yanasababisha wananchi kukata miti kwa ajili ya kupata nishati hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la HELVETAS Daniel Kalimbiya amesema kwa Mkoa wa Morogoro mradi wa USEMINI unatekelezwa katika Halmashauri 4 ambazo ni Mvomero, Ulanga, Malinyi pamoja na Halmahsauri ya Morogoro DC ambapo utazifikia kaya zaidi ya 2000 zenye wanufaika 10000 kata 20 na vijiji 70 katika Halmashauri hizo.
Hata ivyo Kalimbiya amesema Mradi huo utawajengea uwezo wananchi namna ya kusimamia misitu, namna ya kupanga matumizi bora ya ardhi, namna ya kutumia nishati mbadala, pia mradi huo imekusudia kupanda miche milioni moja ya matunda mbalimbali ili kusaidia kurudisha hali ya kawaida yale maeneo ambayo yameathirika na uharibifu wa mazaingira.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.