Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 300 kwa ajiri ya ujenzi wa bwawa la Kidunda ambalo litaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es salaam.
Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 13 mwaka huu na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Felix Kavejuru Mbunge wa jimbo la Buhigwe baada ya kamati hiyo kutembelea eneo la mradi lililopo katika Tarafa ya Ngerengere, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa lengo la kuona hatua ya ujenzi iliyofikiwa.
Mhe. Kavejuru amesema bwawa hilo ambalo lilitakiwa kujengwa toka mwaka 1955 bila mafanikio lakini Mhe. Samia Suluhu Hassan ameamua lijengwe ili kuondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa mikoa mitatu ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
“...tunampongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania... yeye ni jasiri ameamua kwa dhati kutatua changamoto ya maji katika Mkoa huu wa Morogoro na kwa Mkoa wa Dar es Salaam...” amesema Mhe.Felix Kavejuru.
Aidha, Kamati hiyo imeipongeza Serikali kwa mikakati ya kupunguza changamoto ya kukosa umeme kwa wakazi wa eneo la mradi unaotarajiwa kuzalisha umeme Megawati 20 kati ya hizo KV 33 utasambazwa kwa vijiji vinne vya eneo la mradi na mwingine kuingizwa katika gridi ya Taifa hivyo kuchochea ukuwaji wa viwanda nchini.
Kamati imeuagiza uongozi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Morogoro kuhakikisha vyanzo vya maji vinavyolisha bwawa hilo vinalindwa ili kuwa na uhakika wa maji ambayo ndiyo uhai wa bwawa hilo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema bwawa la kidunda ni miongoni mwa jitihada za Serikali za kuvuna maji ya mvua ili kuwa na uhakika wa maji katika kipindi chote cha mwaka huku akibainisha kuwa ujenzi huo ambao tayri umefikia asilimia 15 unatarajia kukamilika ifikapo Juni 2026.
Ameongeza kuwa, wakazi wa maeneo ya mradi ambapo kuna vijiji zaidi ya vinne watakuwa wakwanza kunufaika na mradi huo ili kuwaondolea adha ya kutumia maji chumvi.
Naye Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Christian Gava amesema bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji kipindi cha mvua zaidi ya lita za ujazo bilioni 190 litakuwa na urefu wa mita 870 na kina cha mita 21. Mradi huo umetoa ajira 326 ambapo asilimia kubwa ni wakazi wa maeneo ya mradi unapojengwa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.