Maafisa Elimu wa Mikoa hapa nchini wameagizwa kuhakikisha shule zote za Sekondari katika Mikoa yao zinaunda vikundi vya Skauti ili kuhakikisha uzalendo unajengeka na kuongezeka kwa vijana kwa lengo la kusaidia kuokoa majanga mbalimbali yanayojitokeza katika mazingira ya shule na kupunguza uhalifu unaofanywa miongoni mwao kutokana na kukosekana kwa uzalendo.
Agizo hilo la Serikali limetolewa Disemba 20 mwaka huu na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ndugu Gerald Mweri wakati akifunga mafunzo ya siku Tano ya Walimu Walezi wa Skauti katika shule za Sekondari yaliyofanyika Ukumbi wa VETA Mkoani Morogoro na kushirikisha walimu 100 kutoka Halmashauri 75 za Mikoa 16 Tanzania Bara.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Gerald Mweri, akiwahutubia Walimu walezi wa Skauti (hawapo pichani)
Naibu Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania Abdallah Sakasa (kushoto) akimkabidhi Naibu Katibu Mkuu Gerald Mweri moja ya vitabu vinavyohusu masula ya Skauti. anayeshuhudia ni Mkurugenzi wa Elimu Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia Paulina Mkonongo.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema ni ukweli usiopingika kuwa wanafunzi ambao wako katika vikundi vya Skauti, wamekuwa wakionesha tabia za uzalendo zaidi ukilinganisha na wanafunzi ambao hawajajiunga na skauti ambapo husaidia yanapotokea majaga mbalimbali yakiwemo ya moto hivyo kuokoa uhai wa watu na mali zao. Amesema, Serikali kwa kulitambua hilo, imetoa Waraka unaoagiza shule zote za Sekondari hapa nchini kuazisha vikundi vya Skauti ili kuongeza Uzalendo kwa vijana wa kitanzania hususani wanaopitia shule za Sekondari.
“maelekezo yangu kwa Maafisa Elimu wa Mikoa ni kuhakikisha wanatekeleza Waraka namba Nne wa mwaka 2015 kuhakikisha shule zote zinakuwa na vikundi vya skauti” alisema Naibu Katibu Mkuu Gerald Mweri
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Gerald Mweri akisalimiana na Afisa Vijana Mkoa wa Morogoro Winnifrida Madeba, mara baada ya hafla hiyo.
Aidha, kiongozi huyo ngazi ya kitaifa, amewaasa Walimu waliopata mafunzo hayo ambao ndio walezi wa Skauti katika shule zao, kutojihusisha na matendo yanayokiuka maadili ya Taifa lao, yakiwemo ya wizi wa mitihani, kuiba mali za shule kwa jumla kutokuwa sehemu ya vikundi hivyo bali kuwa sehemu ya kufichua uovu unaotokea katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Gerald Mweri ameagiza shule zote kuwa na utaratibu wa kuiheshimu Bendera ya Taifa, kuipandisha na kuishusha kwa wakati, kwa lengo la kufundisha watoto kuheshimu bendera ambayo ni nembo ya Taifa, pia kuheshimu utaifa wao kwa kuwa Bendera ndicho kielelezo kikubwa cha Taifa.
Baadhi ya Walimu Walezi wa Skauti wakimsikiliza Mgeni rasmi wakati wa kufunga Mafunzo yao
Baadhi ya Walimu ambao pia ni Walezi wa Skauti wakionesha ukakamavu wao wakati wa kuimba wimbo wa taifa
Mwisho, Naibu Katibu Mkuu amesema ili kuongeza uzalendo na historia ya nchi yetu kwa wanafunzi ni vema kabla ya kuingia madarasani, wanafunzi wakawa na nafasi ya kuimba nyimbo za kizalendo ukiwemo wimbo wa Taifa, wimbo wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC, na kwa wakati mwingine kufundishwa nyimbo kama Tanzania nchi yenye furaha, Tanzania nakupenda na nyingine nyingi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia Paulina Mkonongo amesema kuna kwamba shule yoyote yenye kikundi cha Skauti ina nidhamu ya hali ya juu, hata hivyo amesema changamoto iliyojitokeza ni baadhi ya skauti kutojua vema miapaka yao, hivyo kutokana na kuaminiwa kwao katika maeneo yao, baadhi ya skauti walianza kutumia nafasi hizo vibaya na kuwaadhibu hata wanafunzi wenzao jambo lililowashtua na kuwaita walimu walezi ili kuwapa mafunzo ya kwenda kuwaelekeza skauti kuwa kazi yao ni kushawishi wanafunzi wenzao kuwa na uzalendo na nidhamu na sio kutafuta madaraka.
Mkurugenzi wa Elimu Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia Paulina Mkonongo
Nae Naibu Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania Abdallah Sakasa ameiomba Serikali kukarabati majengo ya Kambi Kuu ya Taifa ya Skauti ya Bahati Camp iliyopo katika milima ya Uluguru, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo, huku akieleza kuwa majengo ya Kambi hiyo kwa sasa yamechakaa sana yanahitaji kukarabatiwa.
Naibu Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania Abdallah Sakasa
Pia Naibu Kamishna huyo ameiomba Serikal kuendelea kusaidia kutoa mafunzo hayo kwa Walimu Walezi wa kutoka Halmashauri nyingine zilizobaki ili wanafunzi ambao wapo kwenye vikundi vya skauti inapotokea hitaji la kuhama kutoka shule moja kwenda nyingine huko wanakohamia wakute pia kuna walimu walezi wa skauti, hiyo itasaidia Skauti hao kutomezwa na makundi yasiyokuwa na malezi ya skauti na yeye kutumbukia kwenye makundi hayo yasiyo ya kizalendo.
Nao wafaidika wa mafunzo hayo akiwemo Mwalimu Maria Hoza wa shule ya sekondari ya Shambarai Wilayani Lushoto Mkoani Tanga amewataka walimu wenzake kuwa na tabia ya kuwasikiliza wanafunzi kabla ya kutoa adhabu kwani kusikiliza tatizo la mwanafunzi kunajenga zaidi na kupata majibu ya uhakika namna ya kuwasaidia wanafunzi wao.
Mwalimu Maria Hoza wa shule ya Sekondari ya Shambarai Lushoto Tanga akitoa maneno machache ya shukrani wakti wa tukio hilo.
Jumla ya walimu 100 walioshiriki mafunzo hayo, 22 kati yao walikuwa wamejiunga na vikundi vya skauti na 78 walikuwa hawako kwenye vikundi hivyo. Hata hivyo, baada ya mafunzo hayo ya siku tano kutolewa walimu hao 78 waliridhia kujiunga na Skauti na tayari wamekwishaapishwa kuwa Skauti na sasa pamoja na kwamba wanakwenda kuwa Walimu Walezi wa vikundi vya Skauti katika maeneo yao, wao wenyewe pia wamekuwa ni Skauti ili kuendeleza uzalendo wao kwa wengine.
Ni baadhi ya Maafisa kutoka Ofisi Rais TAMISEMI walioratibu Mafunzo hayo
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.