Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imesema imejipanga kuendelea kuwasogezea karibu huduma za kijamii ikiwemo sekta ya Afya wananchi walio maeneo ya pembezoni ili kurahisisha kutofuata huduma hizo kwa umbali mrefu hivyo kuchochea maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imebainishwa Septemba 29, 2024 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joseph Masunga wakati wa ziara yake pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya Mkoa huo kwa lengo la kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Mkoa huo, na leo ni siku ya tatu wakiwa Wilayani Ulanga.
Mhandisi Masunga amesema, ilani ya CCM inaitaka serikali kuhakikisha inasogeza huduma za kijamii zikiwemo huduma za Afya, Elimu, Maji, miundombinu ya Barabara na umeme na sekta nyingine kwani amesema huduma hizo ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya wananchi.
"… serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba inapeleka huduma za kijamii karibu zaidi na wananchi na moja ya huduma ya msingi sana ni huduma ya afya…" amesema Mhandisi Joseph Masunga
Akiwa katika mradi wa Daraja la Chigandugandu lililopo Wilayani Ulanga, Mhandisi Joseph amewataka wananchi kulinda miundombinu ya umma likiwemo Daraja hilo huku akiwashauri kupanda miti ama mazao kama michikichi, mianzi na Migomba pembezoni mwa mto ili kulinda Daraja hilo ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu Tsh. Mil. 107.
Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kujiandikisha kkwenye daftari la kudumu la kupiga kura ili kujihakikishia kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, 2024 kwani, amesema, hiyo ni haki ya kila mtanzania kupiga kura, kuchaguliwa kuwa kiongozi au kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa huo Bw. Deogratius Mzelu amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Ulanga kwa kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo baada ya wananchi hao kuchangia zaidi ya Tsh. Mil. 12 kwenye ujenzi wa shule ya Sekondari ya Lukande.
Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Lukande Bw. Godfey Senjele amesema ujenzi wa shule hiyo umesaidia kupunguza adha ya wanafunzi wa shule ya Sekondari hiyo iliyopo kata ya Mwaya ambapo walikuwa wanatembea umbali wa 21km kwenda kupata elimu katika sekondari hiyo.
Mwisho
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.