Serikali yafuta mashamba pori 11 Kilosa.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefuta mashamba pori 11 Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro yenye jumla ya Ekari 24,119 na kuyarejesha kwa wananchi ili kuyatumia katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo kilimo na ufugaji.
Taarifa ya kufutwa mashamba hayo imetolewa Juni 7, mwaka huu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (MB) wakati wa ziara yake Wilayani humo iliyolenga kurejesha mashamba pori hayo kwa wananchi yaliyobatilishwa na Serikali baada ya kuona hayaendelezwi.
Waziri William Lukuvi (MB) akiongea na wananchi wa Kilosa wakati wa Mkutano wa hadhara Juni 7 mwaka huu
“Mwezi wa Nne mwaka huu imempendeza Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuyafuta mashamba 11 yenye ekari 24,119, na amenituma nije nitoe maelekezo kwamba baada ya kuyafuta mashamba hayo wizara yangu itaunda timu ya wataalamu kuja kufanya tathimini ya mashamba hayo’’ amesema Mhe. Lukuvi.
‘’.. mashamba yaliyofutwa sehemu watapewe wananchi ambao hawajawahi kumiliki Ardhi na sehemu nyingine watapewa wawekezaji ambao ni waaminifu na hayatagawiwa ovyo.. amesisitiza Mhe. Lukuvi
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa Profesa Paramagamba Kabudi akieleza jambo wakati wa Mkutano huo
Aidha, Waziri Lukuvi amesema mashamba mengine 49 yenye ukubwa wa hekari 45,788.5. yamehuishwa, huku akiwataka wananchi kutovamia mashamba yaliyofutwa kwani watapatiwa kwa utaratibu utakaowekwa mara baada ya kazi ya upimaji kukamilika itakayofanywa na timu ya wataalamu itakayoundwa na akawataka wenyeviti wa vijiji na chama wahakikishe wanatoa ushirikiano wa kutosha katika kusimamia ugawaji wa mashamba hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema licha ya Mkoa huo kuwa na migogoro ya Ardhi, ameweka mipango mkakati ya kuhakikisha Migogoro hiyo inaisha ama kupungua na kuufanya Mkoa huo kusifika katika shughuli za maendeleo badala ya kuwa na migogoro ya ardhi muda wote. “watu waamini kwamba Kilosa, Morogoro ni sehemu salama na watu wanaweza kufanya shughuli zao za kimaendeleo” amesema Mhe. Shigela.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Reuben Shigella akitoa nasaha kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa kabla hajamkaribisha mgeni wake Waziri Mhe. William Lukuvi - Juni 7, 2021
Naye, Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa Profesa Paramagamba Kabudi amesema maamuzi yaliyochukuliwa na Mhe. Rais ya kufutwa kwa mashamba hayo yataweza kupata wawekezaji wenye tija ndani ya Wilaya ya Kilosa na kusaidia Wilaya hiyo kukua zaidi kiuchumi.
Profesa Kabudi
Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa Yohana Kasitila na Kamishna Msaidizi wa Ardhi kanda ya Mashariki Frank Minzikuntwe.
DC Kilosa Adam Mgoyi akiteta jambo na RC wake Martine Shigella
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.