Serikali Mkoani Morogoro imeweka mpango mkakati wa kutoa Elimu kwa wananchi ili kukabiliana na ugonjwa wa vikope {Trachoma} utakaonusuru zaidi ya watu 800 katika Halmashauri za Morogoro na Gairo.
Hayo yamebainishwa May 7, 2021 na Meneja Mpango wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr. George Kabona wakati wa hafla ya kuzindua mpamgo wa kutokomeza ugonjwa huo na kukabidhi vifaa tiba na dawa vitakavyotumika wakati wa uchunguzi na upasuaji wa macho kwa waathirika wa ugonjwa huo, iliyofanyika katika ukumbi wa CATE HOTEL katika Manispaa ya Morogoro.
Dr. Kabona amesema mpango wa taifa ni kutoa Elimu na kuhamasisha jamii kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi ili jamii kujikinga na magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwepo ugonjwa wa Vikope.
‘’Tunapanga kuimarisha mkakati huu kwa nguvu zetu zote katika upande wa kufanya upasuaji, usafishaji wa vikope, lakini pia kunawa uso, kurahisisha upatikanaji wa maji, kuboresha mazingira na usafi wa mwili kwa ujumla tunaamini tukifanikiwa eneo hilo tutakuwa tumefikia malengo yetu ya kutokomeza ugonjwa wa Vikope’’ amesema Dr. George.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema matibabu ya ugonjwa wa Vikope yatatolewa bure kwa waathirika hao huku akiwasisitiza wananchi kuzingatia usafi wa mazingira ili kujikinga na wadudu waenezao ugonjwa huo.
Aidha, Mhandisi Kalobelo ametoa rai kwa wananchi na viongozi watakaoshiriki kutoa matibabu ya ugonjwa huo, kuwashirikisha viongozi katika maeneo husika wakiwemo wenyeviti wa Vijiji, vitongozi na viongozi wa kaya ili kupata mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. SirielMchembe na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Rehema Bwasi wamesema mradi huo wa Sight Saver utasaidia wananchi wa Wilaya hizo kupata matibabu kwa haraka na kuondoa au kupunguza ugonjwa huo katika maeneo yao.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.