Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imekanusha juu ya uwepo wa uhaba wa sukari hapa nchini na kutoa bei elekezi kwa wauzaji wa bidhaa hiyo ambapo sukari itauzwa kwa Tsh. 2800 hadi 3200 kwa kila kilo moja, hivyo imewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika kwa wale wanaokiuka agizo hilo.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Jokate Mwegelo (kushoto) wakimsikiliza mtaalam kutoka kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa mashine na zana za kilimo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipotembelea banda la Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ikiwa ni muendelezo wa maonesho na Sherehe za Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Dkt. Kijaji amesema hakuna upungufu wa sukari hapa nchini kutokana na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hiyo, hivyo amewaelekeza wafanyabiashara wote hapa nchini kuuza sukari kwa bei elekezi ya Tsh. 2,800 hadi 3,200 kwa kilo na kwamba yule atakayekiuka agizo hilo la serikali atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa wawakilishi wa kikundi cha wajasiliamali wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni baada ya kutembelea banda hilo.
“...niwaambie watanzania wawe na amani hatuna upungufu wa sukari na bei ya sukari ni ile ile 2,800 mpaka 3,200, hakuna popote ambapo utaenda utauziwa sukari Tsh. 4,000 ukiuziwa 4,000 toa taarifa sisi tushughulike na huyo anayekuuzia sukari 4,000...” amesema Dkt. Ashatu Kijaji.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimsikiliza Meneja wa idara ya uelimishaji kutoka Bodi ya sukari.
Aidha, Waziri Kijaji ametoa wito kwa viwanda vyote vinavyozalisha sukari hapa nchini kuongeza uzalishaji na uwekezaji kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya sukari ndani na nje ya nchi.
Aidha, Waziri huyo amesema Serikali inaagiza zaidi ya asilimia 60 ya mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi, hivyo amewataka wakulima hususan wanaozalisha malighafi ya viwanda vya mafuta ya kupikia kuongeza uzalishaji huo kutokana na uwepo wa viwanda vya mafuta 771 kwa kufanya hivyo Serikali itapunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.
Sambamba na hilo, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Serikali itawafikia wajasiliamali ambao wamekidhi vigezo vya kupata nembo ya utambulisho (tbs) itawapatia bila malipo yoyote lengo ni kuwasaidia kupata masoko zaidi ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akisalimiana na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.
Leo ni siku ya sita tangu kufunguliwa kwa maonesho hayo Agosti 1, 2023 na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda huku kaulimbiu yake ikiwa ni “Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.