Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt Ashatu Kijaji (Mb.) amesema serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina mpango madhubuti wa kisera, kisheria na kiutaratibu kushirikiana na Taasisi binafsi ili kutatua changamoto wanazopata na kufufua viwanda.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima wakati wa kikao na wafanyabiashara.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo Agosti 11, 2023 wakati akifanya kikao na wafanyabiashara katika ukumbi wa mikutano wa Morena hotel uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kusikiliza changamoto zao za kibiashara na kuzitafutia ufumbuzi.
"... Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alidhihirisha hadharani kwamba Uchumi wa Taifa letu utajengwa na sekta binafsi... kati ya watanzania Milioni 61.7, walioajiriwa na serikali ni milioni 1 tu na milioni 60.7 waliobaki ni kutoka sekta binafsi..." Amesema Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.
Kwa sababu hiyo amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka na inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kushirikiana na Sekta hiyo kwa kuondoa changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na utitiri wa kodi zisizo na maana.
Katika hatua nyingine Waziri Kijaji amebainisha kuwa dhamira ya Serikali ni kurudisha iliyokuwa Mikoa ya viwanda kuendelea kuwa mikoa ya viwanda kama hapo awali ukiwemo mkoa wa Morogoro ili kuweza kutoa ajira kwa vijana wengi na watanzania wasio na ajira Serikalini na kubainisha kuwa sekta binafsi zina nafasi kubwa katika kukuza biashara na uchumi wa Taifa.
Dkt. Kijaji pia ameishauri Mamlaka ya mapato Tanzania -TRA kutowabebesha mizigo isiyo ya lazima wafanyabiashara kwa kulimbikiza kodi bali ameitaka TRA ishirikiane na wafanyabiashara hao na kuwapa elimu kuhusu ulipaji wa kodi badala ya kufungia biashara zao lengo ni kuitaka Serikali kukusanya kodi kwa wingi na wafanya biashara kulipa kodi hizo bila shuruti baada kupata elimu ya ulipaji huo wa kodi.
Akisisitiza kuhusu sekta binafsi kuiwekea mazingira mazuri Dkt. Kijaji amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imerekebisha sheria Na.13 zilizokuwa na changamoto kwa wafanyabiashara lengo ni kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara hao na kukabidhi uchumi katika sekta hiyo ili uchumi uwe imara ndani na nje ya Nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akimkaribisha waziri huyo, amemshukuru Waziri kwa kutambua mchango wa wafanyabiashara wa Mkoa huo kwani wanafanya kazi kubwa hususan kuendesha viwanda mbalimbali kama vya sukari, tumbaku, viwanda vya nguo,viwanda vya kuchakata mchele na mazao ya aina ya mikunde n.k. huku akiwahakikishia Ofisi yake kuwapa ushirikiano wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuweka ofisi maalum itakayoshughulikia mashauri yao kwa haraka watakapofika ofisini kwake.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa wakati akitambulisha wajumbe wa kikao hicho.
Naye, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro Fadhili Chilombe, amewahakikishia wafanyabiashara kuwa changamoto ya umeme wanayoipata sasa ni ya kipindi kifupi tu kwani amesema ifikapo mwakani mwezi Juni Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan itakuwa imetatua changamoto hiyo kwa kuwa na umeme wa megawati 700.
Aidha, Mhandisi Chilombe ametoa jibu kuhusu suala la ulipaji kodi ya pango kwa kila mita katika jengo moja, amesema wafanyabiashara wanaopitia changamoto hizo wapeleke ofisini kwake changamoto hiyo ili kuchagua mita moja itakayolipia Kodi.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bi. Beatrice Njau.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.