Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi Bil. 26.3 za kitanzania kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya Barabara za Mkoa wa Morogoro huku Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa barabara hizo na kubainisha kuwa serikali imedhamilia kuleta mageuzi ya maendeleo kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akikata utepe mikataba ya Barabara akishikiwa na Meneja wa TARURA Bw. Emmanuel Ndyamukama.
Rc Malima akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya Barabara.
Mhe. Adam Malima amebainisha hayo Septemba 12, 2023 wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya barabara kati ya Wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) na Wakandarasi, yenye thamani ya shilingi Bil. 26,377,060,200.00 kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima (hayupo pichani).
Amesema, wananchi wanatakiwa kutambua mchango mkubwa unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita wa kuwafikia watanzania wengi kwani mikataba kama hiyo inalenga kuwaletea maendeleo yao kupitia ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya miundombinu ya barabara, huku akiwataka wakandarasi waliosaini mikataba kukamilisha miradi yao kwa muda uliopangwa ili kuepuka ongezeko la gharama kwa miradi waliyoisaini.
"... lazima tufike sehemu tutambue mchango wa Serikali unaofanywa katika kuifikia jamii na watanzania na haya ndio maendeleo tunayotakiwa tuyafikie tukiyasimamia, nasema haya kwa sababu tuna mradi wa barabara wa Tsh Bilioni 26.3 nimewaambia miradi inatime framing tukikaa na mradi kwa miezi 8 hadi miezi 18 hujamaliza ni disaster..." amesema Mhe Adam Malima.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amewataka viongozi wa Mamlaka ya mapato Tanzania - TRA kutoa mapema vifaa vya ujenzi vinavyopita bandarini ili kuondoa changamoto hiyo ambayo imekuwa ni kisingizio kwa baadhi yao cha kutokamilisha miradi yao huku Afisa usimamizi wa Kodi idara ya elimu na mawasiliano wa Mkoa huo Bw. Lutufyo Mtafya akiahidi kulifanyia kazi agizo hilo.
Sambamba na hilo, Mhe. Malima amesema utekelezaji wa miradi hiyo unahitaji umoja na ushirikishwaji hivyo amewaomba wahe. Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Madiwani, viongozi wengine na wananchi kwa jumla, kushirikiana na kuona kuwa miradi hiyo siyo ya Serikali ni miradi yao hivyo kuisimamia na kuilinda.
Kwa sababu hiyo, amewataka Wakandarasi hao waliotia saini mikataba hiyo watakapokifika kwenye maeneo yao wawashirikishe wadau wote muhimu katika utekelezaji wa miradi hiyo na hivyo kuwafanya kuwa ni miradi yao (ownership).
Awali, Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Bw. Emmanuel Ndyamukama amesema fedha hizo Bil.26.3 zimelenga kufanyia matengenezo mbalimbali ya barabara, fedha ambazo zitatoka katika mfuko wa barabara Tsh. bilioni 8.6, fedha za tozo Tsh. Bil. 12.2 na fedha za mfuko wa Jimbo Tsh. Bil. 5.5 na kuleta jumla ya Tsh. 26.3 ambapo fedha hizo zitakazotumika kutengeneza barabara na kuunganisha maeneo yote yenye shughuli za kiuchumi kama kilimo, Utalii na madini.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Bw. Emmanuel Ndyamukama akitoa taarifa kuhusu mikataba hiyo ya barabara.
Nae Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wote Mkoa wa Morogoro, kwa niaba yao, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha Sh. Bil. 26.3 Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kuwahudumia wananchi kwenye sekta hiyo ya miundombinu.
Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Morogoro akitoa salamu za Wabunge wa Mkoa huo katika hafla hiyo.
Aidha, ametaka Wakandarasi waliopewa tenda ya ujenzi wa barabara mkoani humo, kutekeleza miradi hiyo kwa ubora unaotakiwa huku akiwataka kubadilika na kufanya kazi zao kwa umahili ili tenda hizo waendelee kupewa wao kama wazawa badala ya wageni.
Amesema, ni jambo la kusikitisha wakandarasi wa kitanzania wakipewa kazi na wakandarasi wageni kufanya kazi kama wahandisi wanafanya kazi nzuri sana, lakini wakiaminiwa na kupewa kazi hizo kama wakandarasi hawafanyi vizuri na kuwataka wabadilike ili kazi nyingi za ukandarasi hapa nchini wapewe watanzania wenyewe.
TARURA itaingia Mikataba na Wakandarasi 82 yenye thamani ya jumla ya zaidi ya Tsh. Bil. 26.3 ambapo leo imesainiwa mikataba 23 yenye thamani ya shilingi Bil. 6.13 huku mikakati ya TARURA Mkoa wa Morogoro ili kufikia malengo wamedhamiria kudhibiti muda wa utekelezaji miradi, kudhibiti gharama, kudhibiti ujenzi wa viwango na kuhakikisha wadau wote muhim wanashirikishwa.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.