Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoshughulikia Elimu, Utamaduni na Michezo imeishauri Serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya utafiti iliyopo hapa nchini.
Ushauri huo umetolewa Machi 15 mwaka huu na Mhe. Kitila Mkumbo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge inayohughulikia Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa ziara ya kamati hiyo walipotembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo Mkoani Morogoro.
“… nitoe wito wetu kama bunge, kuendelea kuiomba serikali kutoa fedha za utafiti ili chuo hiki kiendelee kufanya utafiti na ugunduzi mkubwa na kujiimarisha Zaidi…” amesema Mhe. Kitila Mkumbo.
Aidha, Mhe. Mkumbo amesema wamefurahishwa jinsi chuo hicho kilivyojipanga kutoa wanafunzi mahili na wenye uwezo wa kujitegemea pale watakapohitimu masomo yao.
Wakiwa chuoni hapo, kamati imekagua vitengo vya mafunzo kama kituo cha utafiti na mafunzo ya uchumi wa bluu, hospitali ya Taifa ya rufaa ya Wanyama na jengo mtambuka la mafunzo kuona namna mafunzo kwa vitendo yanavyofanyika na utafiti wa miradi hiyo inavyofanya kazi na kuongeza pato kwa chuo na Taifa kwa ujumla.
katika hatua nyingine Mhe. Mkumbo ametoa wito kwa wanafunzi wa shule hapa nchini kujikita katika masomo ya sayansi na kwenda Kusoma vyuo vilivyojipanga vema katika kutoa wahitimu mahili kama Chuo Kikuu cha SUA.
Kwa upande wake, Mhe. Omari Juma Kipanga ambaye ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema serikali ina mpango mkakati wa kutekeleza mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transfomation) utakaogharimu Zaidi ya Tsh. Bilioni 972, fedha hizo zitapelekwa katika vyuo vyote nchini kushughulikia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Waziri Kipanga ametumia fursa hiyo kupongeza jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. DK. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya Tsh. Bilioni 11 kwa ajili ya ujenzi wa jengo linalochukua wanafunzi zaidi ya 300 katika chuo cha SUA.
Nae, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael T. Chibunda amesema kupitia mradi wa HEET chuo kimenufaika kupewa Tsh. Bilioni 73.6 kwa ajili ya kupanua na kuboresha mradi huo wa miaka 5 ulioanza mwaka 2022.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.