Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imesema iko mbioni kubadilisha mitaala ya Elimu na kuhakikisha SANAA na MICHEZO yanakuwa masomo maalum lengo ni kukuza vipaji vilivyopo katika sekta hizo, hivyo kutoa ajira nyingi kwa vijana kupitia sekta hizo.
Hayo yamebainishwa Agosti 16 mwaka huu na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Pindi Chana alipotembelea kituo cha kukuza vipaji vya mpira wa miguu (Morogoro kids) kilichopo uwanja wa Mashujaa Mkoani Morogoro ikiwa ni ziara yake ya kikazi Mkoani humo.
Mhe. Balozi Pindi Chana amesema serikali imedhamiria kubadilisha mitaala ya elimu kwa kutaka masomo ya Sanaa na Michezo kuwa masomo maalum ambapo vijana watafanya michezo hiyo na kujuza vipaji vyao sambamba na kufanya kazi hiyo kwa stadi na weledi mkubwa zaidi.
Mhe. Balozi Pindi Chana akipokea jezi kutoka vijana wa kituo cha Moro kids.
"... ndugu zangu, Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo tumedhamiria kuhakikisha suala la michezo nchini linapewa kipaumbele, hivi sasa tuko katika hatua ya kubadilisha mitaala ya elimu, tunataka masomo ya sanaa na michezo yawe masomo maalum ili tuendelee kukuza vipaji tulivyonavyo..." Amesema Mhe. Balozi Pindi Chana
Aidha, Mhe. Pindi Chana ameagiza kamati za Wilaya na Kamati ya Mkoa wa Morogoro kukutana ili kujadili changamoto zinazoikabili michezo katika eneo husika ili kutafuta namna ya kutatua changamoto hizo.
Sambamba na hilo, Mhe. Balozi Pindi Chana amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya michezo kwani amesema ameonesha njia na kuwa mfano mzuri na kuifanya Tanzania kuanza kunga'ara kimichezo.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Pindi Chana akiwa pamoja na Viongozi wa Mkoa na Wilaya wametembelea uwanja wa Jamhuri Mkoani humo ili kukagua maendeleo ya maboresho yanayoendelea.
Aidha, Waziri huyo amezipongeza sekta binafsi hususan Taasisi za benki zinavyozidi kumuunga mkono Rais katika suala zima la michezo kwa kuanzia michezo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameipongeza timu ya Young Africans sports club (Yanga) mabingwa wa kihistoria kwa kujitokeza na kukifadhili kituo hicho cha Moro Kids cha kukuza vipaji hususan mchezo wa mpira wa miguu kwani amesema hatua hiyo itaondoa changamoto ya vifaa kama mipira, jezi n.k na fedha za kuendeshea kituo hicho ambazo zilikuwa zinakikwamisha kituo hicho kufikia malengo yake kikamilifu.
Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mstahiki Meya wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Pascal Kihanga kutafuta eneo zuri na kukitoa kwa kituo hicho cha Moro kids kwa ajili ya kujenga kiwanja cha michezo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiteta jambo na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga.
Naye, Mkurugenzi wa kituo cha Moro kids Prof. Madundo Mtambo ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutembelea kituo hicho na kuomba eneo ili kuwa na viwanja vya michezo vitakavyo weza kukidhi vijana wengi, kwani kwa sasa wanaopata nafasi ya kupata mafunzo sambamba na mazoezi ni vijana wachache.
Kituo hicho cha kukuza vipaji vya michezo cha Moro Kids kilianzishwa 1999 na kusajiliwa mwaka 2004 na Baraza la michezo Tanzania.
Hadi sasa kituo kimepata mafanikio makubwa kwa kukuza vipaji vya wachezaji wanaozitumikia timu zao kama Dickson Job, Abtwalib Msheli Kibwana Shomari, Dickson Kibabage, na Zawadi Mauya wakiwa timu ya Yanga na Shomari kapombe na Mzamiru Yasin kutoka timu ya Simba, hivyo ni kituo hicho kinakuza vipaji kwa ajili ya manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.