Serikali yatatua Mgogoro wa wananchi wa Mindu, 357 kulipwa kifuta jasho.
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemaliza mgogoro wa muda mrefu wa Kata ya Mindu, kwa kuwalipa kifuta jasho wananchi 357 na wengi wao kuruhusiwa kubaki katika makazi yao lakini kwa kufuata miongozo ya Serikali ili kulinda Bwawa la Mindu ambalo ni tegemeo la wananchi wa Manispaa ya Morogoro katika upatikanaji wa maji.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Septemba 22, 2023 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry William Silaa (Mb) alipofanya ziara ya siku moja Mkoani Morogoro na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Mindu ili kutatua mgogoro uliokuwa unaleta mvutano baina ya wananchi na Serikali.
Akitoa kauli hiyo, Waziri Jerry Silaa amesema kwa mujibu wa nyaraka za Wataalam zilizopo, tayari watu waliokuwa wanaishi eneo la Bwawa la Mindu miaka ya 1979 walishalipwa fidia na walielekezwa Kwenda eneo la Mafuru Wilayani Mvomero, hivyo kwa sasa hakuna mwananchi anayestahili kulipwa fidia tena isipokuwa wananchi 357 kupewa kifuta jacho.
Akibainisha zaidi Mhe. Waziri amesema wananchi 357 wanaostahili kupewa kifuta jasho na kuondoka eneo la Mindu ni wale wanaoishi ndani ya Mita 500 kutoka Bwawani na walio nje ya mita hizo wataendelea na makazi yao lakini kwa kufuata miongozo yote itakayotolewa na Serikali kwa lengo la kulilinda Bwawa hilo kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mhe. Waziri amesema, Pamoja na kuwapatia kifuta jasho wananchi 357 wanaotakiwa kuhama, bado Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa busara zake amewataka wananchi hao kuwpatia kiwanja kimoja kila mmoja katika eneo la CCT ili wakaendeleze Makazi yao eneo hilo.
"Dkt. Samia amenielekeza kwa utaratibu ule ule wa hekima, busara na huruma yake kwa wananchi 357 nikuelekeze Kamishna Msaidizi wa Ardhi kuhakikisha wanapata viwanja na huo uwe mkono wa heri kwao ili tulinde hili bwawa Kwa faida yetu..." amesema Mhe. Jerry Silaa.
Hata hivyo, Waziri huyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na huruma, busara na hekima kwa watu wake, na kuonya vikali wananchi watakaokiuka taratibu hizo hekima haitatumika tena bali sheria zitafuata mkindo wake.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akimkaribisha Mgeni wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema yupo tayari kupokea maelekezo yote kutoka serikalini na kuyasimamia kama miongozo inavyoelekeza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro Bw. Frank Minzikuntwe amewasihi wananchi waliobaki ambao wako nje ya mita hizo 500 kuheshimu na kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kutoendeleza maeneo hayo huku akisikitishwa na baadhi yao kuendelea na ujenzi wa makazi rasmi kabla ya kurasimishwa maeneo hayo.
Sambamba na hayo Bw. Frank amewataka wananchi hao kuwa wavumilivu kutoendeleza makazi yao hadi hapo watakapomaliza zoezi la urasimishaji Ardhi linalotarajiwa kuanza hivi karibuni ili kuepusha migogoro ya Ardhi ya mara kwa mara inayojitokeza Mkoani Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.