Serikali yatenga 1.2 Bil. kwa ajili ya ujenzi wa gati
Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kujenga gati mbili kwenye mto mnyera kwa ajili ya kuweka kivuko kitakachosaidia kuunganisha wilaya ya Malinyi na Kilombero Mkoani Morogoro na hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Wilaya hizo mbili.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela {mwenye kofia katikati}akiwa eneo la ujenzi wa gati la Mto mnyera upande wa Wilaya ya Malinyi
Akizungumzia faida ya ujenzi wa Magati hayo mawili na kuweka kivuko, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro MARTINE SHIGELA amesema licha ya kusaidia kuunganisha wilaya hizo mbili lakini ujenzi huo pia kutasaidia kurahisisha mawasiliano ya mikoa miwili ya Morogoro na Njombe.
mto Mnyera
Akibainisha zaidi kuhusu ujenzi huo Martine Shigela amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetenga jumla ya shilingi Bil. 3.2Bil kwa ajili ya ujenzi wa gati mbili kwa maana ya pande mbili za mto Mnyera ujenzi utakaogharimu shilingi 1.2 Bil.
Lakini pia amesema Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini - TARURA wamepewa shilingi 1.5Bil. kwa ajili ya ujenzi wa barabara zitakazounganisha magati hayo mawili kila upande wa mto mnyera yaani gati la kila upande na kisha wataongezewa shilingi 500 Milioni watakazopewa kwa awamu mbili kila awamu shilingi 250Milioni na kufanya jumla ya shilingi 3.2 Bil.
Shigela amebainisha kuwa lengo la Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hasssan kujenga kivuko hicho ni kurahisisha usafirishaji wa mazao ya wananchi wa wilaya hizo mbili na mikoa jirani lakini pia Mkoa wa Morogoro unakwenda kufikia kirahisi mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma kupitia kivuko cha mto Mnyera.
“Upande wa TANROADS tayari wameshatenga fedha 1.2 Bil.watajenga gati huku na watajenga gati upande wa pili ili kuunganisha na kuleta kivuko sit tu kwa ajili ya kusafirisha binadamu bali pia kusafirisha mazao ya kibiashara” amesema Martine Shigela.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mhe. Pius Mwelase (mwenye koti jekundu) akiwa pamoja na baadhi ya viongozi walioambatana na RC katika msafara wake
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka TARURA wa pande zote mbili za Mlimba na Malinyi kuhakikisha kutumia vizuri bajeti ya fedha zilizotengwa ili kuhakikisha barabara hizo zinafunguka, huku akiwataka wananchi kujipanga kuzalisha kisasa na kutumia hiyo fursa inavyotakiwa na kuendelea kulinda na kutunza mazingira ya mto Mnyera kwa kuwa mto huo ni moja ya vyanzo vikuu vya bwawa la kufua Umeme la Mwlimu Nyerere.
Wa kwanza kushoto ni DAS Malinyi na wa pili ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslim
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi PIUS MWELASE amesema kivuko hicho kitasaidia wananchi kwenda mikoa ya jirani kwa shghuli za kijamii ikiwemo kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya Ikonda iliyoko Mkoa wa Njombe lakini pia kivuko hicho kitaongeza mapato ya Halmashauri yao.
Naye Ditram Mhenga Diwani wa Kata ya Utengule iliyoko upande wa pili katika Halmashauri ya Mlimba Wilaya ya Kilombero amesema kukamilika kwa kivuko hicho kutaongeza uchumi wa halmashauri hizo mbili kupanda kwani eneo hilo baada ya kufunguka litavuta wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo ya kilimo.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.