Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt. Ashatu Kijaji (MB) amesema Serikali ya awamu ya sita imetenga fedha shilingi Bil 28.1 kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa ajili ya sekta ya mifugo pekee kwa ajili ya kutekeleza mapinduzi ya sekta hiyo ikiwemo kufanya kampeni ya chanjo ya mifugo ili kuhakikisha mifugo hapa nchini inakuwa na ubora unaohitajika kimataifa.
Waziri Kijaji amesema hayo Januari 4, 2025 Wilayani Mvomero katika Kijiji cha Kambala ambacho ni maalum kwa ajili ya wafugaji ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Morogoro.
Akifafanua zaidi, Waziri Dkt. Ashatu Kijaji amesema, fedha hizo zimelenga kutoa chanjo za homa ya mapafu ya ng'ombe, ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo na ugonjwa wa kuku wa kideli huku fedha nyingine kutumika kununua pikipiki 700 na vishikwambi 4500 kwa ajili ya maafisa ugani wa mifugo ili kurahisisha utendaji kazi wao hivyo kutimiza maono ya Rais Samia.
"...Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 60 tangu tupate uhuru, Mama katupa Tsh. Bil. 28.1 kwa ajili ya wafugaji tu..." amesema Dkt. Ashatu Kijaji.
Aidha, Waziri amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na uvuvi anayeshughulikia Mifugo kufanya utafiti wa haraka ili kujenga kisima au bwawa katika kijiji cha Kambala kabla ya bajeti ya mwaka 2025/2026 ili wafugaji hao kuacha kufuata maji umbali mrefu na kusababisha migogoro baina yao na wakulima.
Katika hatua nyingine, Waziri Ashatu Kijaji amewataka wafugaji kwenda na kasi ya mapinduzi ya sekta hiyo na kutekeleza kwa vitendo utaalamu wanaopewa na maafisa ugani kwani amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhun Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha mapinduzi ya sekta hiyo yanafanikiwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa wa Morogoro una agenda ya mapinduzi ya mifugo kwa kupata mbegu za mifugo hasa ng'ombe ambao watafugwa kisasa na kuondokana na Mkoa kuwa na mifugo mingi isiyo na tija, badala yake kuwa na mifugo michache lakini yenye ubora na inayokidhi masoko ya nje.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amesema migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji Mkoani humo inasababishwa na ukosefu wa maji, kwani amesema wafugaji wanapotafuta maji kwa ajili ya mifugo yao mara nyingi mifugo yao hupata nafasi ya kula mazao ya wakulima hivyo amemuomba Waziri kuchimba kisima kwenye kijiji cha Kambala ili wananchi wake kupata maji ya uhakika kwa ajili ya mifugo yao.
Naye Askofu Jacob Mameo wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa na mchango chanya katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya mifugo kwani amesema migogoro iliyokuwa ikizikumba Wilaya za Kilosa na Mvomero miaka ya nyuma imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za serikali hii ya awamu ya sita.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.