Serikali yaagiza Wizara,Taasisi za Serikali kupanga bajeti kwa ajilia ya SHIMIWI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amewaagiza Viongozi wa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali pamoja na Sekretarieti za Mikoa kupanga bajeti kwa ajili ya watumishi wao wa Umma kushiriki mashindano ya SHIMIWI yanayofanyika kila mwaka hapa nchini.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo leo Oktoba 23 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro wakati akifungua rasmi mashindano hayo ya SHIMIWI yaliyoanza kutimua vumbi Oktoba 20 mwaka huu katika viwanja mbalimbali Mkoani humo.
Makamu wa Rais amesema kwa kuwa kalenda ya michezo ya SHIMIWI inajulikana kila mwaka haoni sababu ya Wizara au Taasisi nyingine za Serikali kutoshiriki michezo hiyo na kuwaelekeza Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali na Makatibu tawala wa Mikoa kupanga bajeti za Ushiriki katika michezo na kuwaruhusu watumishi kushiriki michezo hiyo.
“sasa, kwa kuwa kalenda ya michezo hii inajulikana, ninawaelekeza watendaji Wakuu wote wa Wizara, Idara,Taasisi za Serikali na Sekretarieti za Mikoa kwanza wahakikishe bajeti za ushiriki katika michezo zinapangwa mapema” ameagiza Makamu wa Rais.
“Lakini vilevile wawaruhusu watumishi kujiandaa kufanya mazoezi kwa muda mwafaka ili waweze kujiandaa mashindano ya SHIMIWI yanayofanyika kila mwaka” amesisitiza Dkt Mpango.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewataka wakuu wa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na Sekretarieti za Mikoa ambao hawakushiriki kwenye mashindano ya SHIMIWI ya mwaka 2021 kujieleza kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sababu za kutoshiriki mashindano hayo na nakala ya maelezo yao yapelekwe kwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ndiye Mlezi wa Mashindano hayo.
Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa michezo hiyo na kuwataka washiriki waitumie kwa ajili ya kufahamiana na kujenga urafiki baina yao na matarajio ya serikali kwa watumishi wake katika kushiriki michezo hiyo kutasaidia kujenga uchumi wa Taifa, kuimarisha Afya za wafanyakazi na kujenga tabia ya kupendana na kusaidiana.
Akifafanua zaidi umuhimu wa suala la michezo, Makamu wa Rais amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha kuwa magonjwa yasiyoambukizwa yamesababisha jumla ya vifo vya watu milioni 41 sawa na 71/% ya vifo vyote ambavyo vilitokea duniani mwaka 2016.
Kwa mukhtadha huo, Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania wote kushiriki mazoezi mara kwa mara, kwani mazoezi ni dawa ya miili yetu na husaidia kuiweka miili katika hali iliyo njema zaidi na kuepuka magonjwa hayo ya kuambukiza.
Aidha, amewaagiza wakuu wa Wizara zote, Idara, Taasisi za Serikali na Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha wanaweka utaratibu kwa watumishi wote kufanya mazoezi mara moja kila mwishoni mwa wiki.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema mashindano ya SHIMIWI kufanyika Mkoani Morogoro ni fursa kubwa kiuchumi na kibiashara kwa kuwa wachezaji wa michezo hiyo zaidi ya 1,700 wako katika mji wa Morogoro hivyo hoteli nyingi zimepata wateja pamoja na wafanyabiashara mbalimbali hali inayopelekea ongezeko la mzunguko wa fedha.
Sambamba na hayo Shigela amemwomba Mkamu wa Rais kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa michezo yote ya inayofanyika kitaifa, kwa kuwa mkoa huo uko katikati ya Jiji la Dodoma ambao ni Makao Makuu na Jiji la kibiashara la Dar es Salaam hivyo kuwa rahisi hata kwa viongozi wengine wa kiserikali wanataka kushiriki michezo hiyo kushiriki.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni Dkt. Hassan Abbas amemweleza Makamu wa Rais kuwa kwa sasa Tanzania inafanya vizuri kwenye eneo la michezo akitaja mafanikio mbalimbali zikiwemo timu za mpira wa miguu wakiwemo wanawake yaani timu ya mpira wa miguu ya wanawake nchini - Twiga Stars na timu ya wananwake chini ya miaka 20 kufanya vizuri kwenye mashindano yao.
Kwa sababu hiyo, amewataka waajiri wote wa Taasisi za Serikali kuendelea kujipanga na kuwaruhusu watumishi wa Umma walioko chini yao kushiriki kwenye michezo kama sehemu yao ya kutoa mchango wao kwenye sekta hiyo Muhimu.
Mara baada ya ufunguzi huo wa michezo ya SHIMIWI uliofanywa na Makamu wa Rais, michezo mbalimbali iliendelea KUCHEZWA kama ilivyopangwa likiwemo SOKA ambapo timu ya RAS Morogoro kwa mara ya kwanza na kwa bahati mbaya sana imekubali kichapo cha mabao mawili kwa moja dhidi ya timu ya Kilimo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.