Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini - TASAF imetoa kiasi cha shilingi Mil. 193 kwa ajili ya ujenzi wa wodi moja ya wazazi katika zahanati ya kata ya Mkambarani iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro lengo likiwa ni kuwapunguzia adha ya kutembea mwendo mrefu kutafuta huduma ya Afya.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo Julai 27 mwaka huu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Deogratius Ndejembi amesema kutolewa kwa fedha hizo kunatokana na maombi ya wananchi waliyoyatoa kupitia viongozi mbalimbali wa chama na Serikali juu ya adha wanayopata katika kupata huduma ya Afya.
Aidha, Ndejembi ametoa onyo kali juu ya matumizi sahihi ya pesa iliyotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa wodi hiyo na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando kusimamia vizuri ujenzi huo ili fedha hizo zisitumike kinyume na maagizo ya Serikali.
"Kusitokee mchwa wa kutafuna fedha hizi, hatutamfumbia macho maana wapo baadhi ya watu wakishaona fedha Kama hivi wanawaza kuzitafuna tu, DC simamia ujenzi huu na wasitumike wakandarasi hapa itumike force akaunti" amesema Ndejembi.
Sambamba na hayo, Ndejembi amewataka wenyeviti wa vijiji na mitaa kutenda haki katika uandikishaji wa kaya maskini na kuacha hila wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo ili kila mwananchi anayestahili kuwa katika mpango wa TASAF apate haki yake.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Wilaya ya Morogoro Bi. Austaki Moshi, amesema mpango huo wa kunusuru kaya maskini umeleta manufaa katika Kijiji cha Mkambarani ikiwemo watoto kuhudhuria kliniki na kusaidi wanafunzi kuhudhuria kwa wingi Shuleni kutokana na huduma nzuri zinazotolewa.
Pia Bi. Austaki amesema jumla ya wanafunzi 110 wanasoma na kupatiwa mahitaji ya elimu kwa kutimiza masharti ya mpango huo katika shule ya msingi Mkambarani.
Awali, akiwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mkambarani, Mbunge wa jimbo la Morogoro kusini Hamisi Tale Tale, maarufu kama Babu Tale amesema amekuwa akipata malalamiko mengi kutoka kwa wazee wasiojiweza juu kutoandikishwa katika mpango wa TASAF hali inayopelekea wazee hao kuishi katika maisha ya dhiki.
Naye Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando amekiri kupokea maagizo ya Naibu Waziri huyo na kumuhakikishia kutekeleza maagizo yote aliyoagiza ili kutimiza adhma ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri y Muungano wa Tanzania ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Mpango wa kunusuru kaya maskini - TASAF awamu ya tatu ni mpango wa Kitaifa ambao unatekelezwa Tanzania bara na Zanzibar. Mpango huu ulizinduliwa rasmi na Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 22 Agosti 2012, Jijini Dodoma.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.