Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza ujenzi wa Daraja moja na jingine kukarabatiwa katika Kijiji cha Chigandugandu na Mbuga Wilayani Ulanga Mkoani Morogoro baada ya madaraja ya awali kuathiriwa na Mvua za Elinino za mwaka huu na kusababisha adha kwa wananchi wa maeneo hayo.
Hayo yamebainika Juni 12, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa ziara yake akiambatana na Wajumbe wa KUU ya Mkoa huo ya kukagua miundombinu mbalimbali na utekelezaji wa Maelekezo ya Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) aliyoyatoa wakati wa ziara yake takribani mwezi mmoja uliopita.
Mhe Adam Malima amesema, Waziri Mchengerwa alifanya ziara Mkoani Morogoro kujionea hali ya Mafuriko yalivyoukumba Mkoa wa Morogoro na baada ya kufika eneo la Daraja la Mbuga alitoa ahadi kwa niaba ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga madaraja hayo mawili ya Kamba ili kuwaondolea adha wananchi hivyo amefika kufuatilia utekelezaji wa fedha hizo.
“sisi leo tumekuja kuangalia maendeleo ya kazi ya zile milioni 250 zilizotoka kwa ajili ya kurekebisha haya madaraja mawili” amesema Adam Kighoma Mhe. Malima.
Amesema, uharibifu wa madaraja hayo mawili umechangiwa kwa vikubwa na shughuli za kibinadamu hasa kilimo kinachofanyika pembezoni mwa mto unaojengwa madaraja hayo mawili na akatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutofanya shughuli za kilimo ndani ya mita sitini kila upande wa mto au kulima mazao rafiki yanayozuia mmomonyoko wa ardhi.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala ya Barabara za Mjini na Vijijini – TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emanuel Ndyamkama amesema, madaraja hayo mawili yanajengwa baada ya kupokea fedha kutoka Serikalini na yatajengwa kwa kipimo cha kuwezesha kupita waenda kwa miguu, pikipiki za magurudumu mawili na zile za magurudumu matatu – Toyo pekee ili kurahisisha wananchi kuvusha mazao yao lakini pia kuyafanya yadumu kwa muda mrefu.
Aidha, Mhandisi Ndyamkama amesema Baada ya mafuriko ya Mvua za Elinino za mwaka huu, wamefanya tathmini na kugundua kuwa Mkoa wa Morogoro una uhitaji wa madaraja 64 ya aina hiyo ya madaraja yanayojengwa eneo hilo ambayo thamani yake ni Tsh. Mil. 200 kwa kila Daraja moja la Kamba.
Naye Diwani wa Kata ya Ilonga Habiba Abdallah Katundu kwa niaba ya wananchi wake, amemshukuru Rais kwa kupeleka fedha za kujenga Daraja moja jipya na kukarabati jingine ambayo yote ni ya Kamba, hii ni kutokana na athari za mafuriko kubomoa madaraja hayo, hivyo kukamilisha madaraja hayo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa ambayo ndio kichocheo cha Uchumi wa eneo hilo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.