Serikali imetoa jumla ya shilingi bil. 310 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule 707 hapa nchini ukiwemo ujenzi wa shule mpya, kuongeza vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali za sekondari zenye uhitaji pamoja na ukarabati wa miundombinu mingine ya shule hizo.
Hayo yamebainishwa Julai 24, 2024 na Mwl. Ephreim Simbeye ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teklolojia Prof. Carolyne Nombo wakati akifungua Mafunzo ya siku tatu kwa Maafisa Elimu Mikoa, Halmashauri, Maafisa Tehama, Maafisa ugavi, na Wakuu wa shule za sekondari.
Akifafanua zaidi katika kikao hicho kilichofanyika Chuo cha Elimu ya watu wazima cha Morogoro (WAMO) Mwl. Ephreim Simbeye amesema lengo la kikao hicho ni kutoa uwezo kwa maafisa hao katika usimamizi wa miradi ya shule za Msingi na Sekondari.
”…jumla ya Tsh. Bil. 310 zimetumwa katika shule 707 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari…” amesema Mwl. Ephreim Simbeye
Amebainisha kuwa fedha hizo zitatumika katika kujenga madarasa mapya ya shule za sekondari za wavulana za kanda, shule za kata, upanuzi wa shule kwa ajili ya kidato cha tano na ukamilishaji wa miundombinu ya shule za wasichana za Mikoa, hivyo amewataka Wakuu wa Shule za sekondari na Misingi kuwa wadilifu na waminifu katika kutekeleza miradi mbalimbali ya Serikali.
Sambamba na hilo, Mwl. Ephreim amesema kupitia mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) serikali imedhamiria kuboresha ufundishaji kupitia mpango wa mafunzo endelevu ya Walimu kazini (MEWAKA) ambapo Walimu wa Sayansi na Hisabati wamepatiwa mafunzo ili kuongeza umahiri wa ufundishaji darasani.
Katika hatua nyingine, Mwl. Simbeye amesema serikali imejipanga kuboresha Elimu hapa nchini ikiwemo kuboresha miundombinu ya shule kwa ajili ya kujifunzia na kufundishia ili kuongeza ufaulu, kwani amesema kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa katika shule za msingi na sekondari huku ikionekana kuwa na changamoto ya miundombinu mashuleni hususan vyumba vya madarasa.
Pia amesema serikali ina mpango wa kuingia katika mafunzo ya kidijitali ambapo vifaa vya Maabara na TEHAMA vitasambazwa kwa shule 281 kupitia wazabuni waliopatikana.
Kwa sababu hiyo, Mwalimu huyo amewasisitiza Wakuu wa shule kuhakikisha wanaweka mifumo na mikakati thabiti ya kuwalinda watoto kwa kushirikiana na jamii dhidi unyanyasaji na ukatili wa wanafunzi ndani na nje ya shule kwa kuanzisha vilabu vya wanafunzi kwa ajili ya kujitambua na kujiamini ili kuwa na ujasili wa kueleza wanapopatwa na changamoto kama hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu ya awali na msingi OR – TAMISEMI Mwl. Sussan Nussu amesema Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia imeweka miongozo mbalimbali itakayotumika katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule za serikali lengo ni shule zinazojengwa ziwe zinakidhi viwango bora vilivyokubalika (Value for Money).
Naye, Mratibu wa mradi wa SEQUIP Bw. Richard Makota amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa makundi 6 ambapo kwa sasa wameanza na makundi 3 yanayofanyika katika Mikoa ya Mtwara, Morogoro na Mwanza lengo likiwa ni kufikia mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Halmashauri 184 na shule zilizopokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.