Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha Shilingi Milioni 800 kwa ajili ya kujenga Daraja la mto Furua ili kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji inayowakabili wananchi wa Wilaya hiyo.
Hayo yameelezwa leo Mei 21, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) wakati akiendelea na ziara yake Mkoani humo.
Ni siku ya pili ya ziara ya Waziri Mchengerwa akiwa Mkoani Morogoro ambapo leo Mei 21, 2024 yupo Wilayani Malinyi na kukagua miundombinu ya barabara za Mji wa Malinyi na kujiridhisha kuwa miundombinu hiyo imeharibiwa vibaya na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni na kwa niaba ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Waziri ametoa fedha hizo kwa ajili ya kujenga Daraja la Mto Furua ikiwa ni suluhisho la muda.
Hata hivyo, amuagiza Meneja wa Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Ndyamukama kutafuta mkandarasi wa kujenga Daraja la Mto huo na kukamilisha ndani ya kipindi cha wiki mbili ili kuwawezesha wananchi wa Malinyi kusafirisha nafaka na bidhaa mbalimbali ambazo ni muhimu kwao na kwa Uchumi wa Taifa.
“…nimeshawaelekeza watendaji wa Wizara yangu Mkurugenzi wa Ujenzi TAMISEMI anayewasimamia TARURA na Meneja wa TARURA wameniambia wanahitaji Mil. 800, nimewapa wiki mbili nataka Barabara hii ipitike…’’Amesema Waziri Mchengerwa.
Sambamba na hilo, Mhe. Mohamed amewataka viongozi wa ngazi zote kushirikiana na kuwa wabunifu ili kuwatumikia wananchi kikamilifu huku akiwaagiza Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara kuitisha vikao vya dharura na wataalamu wote ndani ya Mikoa yao pamoja na wadau wa Maendeleo ili kujadili na kurejesha mawasiliano ya Barabara zilizoharibiwa na mafuriko.
Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za dharura kwa lengo la kukarabati miundombinu mbalimbali ikiwemo Barabara kutokana na athari za mafuriko yaliyotokea maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akimkaribisha Waziri huyo wa TAMISEMI, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa maamuzi yake ya haraka kwa kutoa fedha Tsh. Mil.800 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la mto Furua na kuonya kuwa asiwepo kiongozi ama mtu yeyote kujaribu kufuja fedha za Mradi huo ili Daraja litakalojengwa lilingane na fedha zilizotolewa (Value for Money).
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Malinyi Mhe. Said Tila kwa niaba ya wananchi wa Malinyi, pamoja na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumtuma mwakilishi wake kutoa pole za mafuriko na kuona athari zake, amebainisha changamoto wanazozipitia ikiwa ni pamoja na bei za bidhaa kupanda.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.