Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia shilingi 1.2 Bil. kurejesha mawasiliano ya Barabara Wilayani Malinyi Mkoani Morogoro baada ya Mvua za Eli nino kuharibu miundo mbinu hiyo na kuacha mji huo ukiwa kisiwani.
Hayo yamebainishwa Juni 11, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa huo kwa lengo la kukagua miundombinu iliyoathirika na mvua za Elinino ndani ya Mkoa huo.
Akiwa Wilayani Malinyi, kiongozi huyo amewaeleza wananchi kuwa Mvua za Elinino zilileta uharibifu mkubwa wa miundombinu na kusababisha mto Furua kujaa maji na kumwaga katika mji wa Malinyi na kuvunja madaraja muhimu.
Hata hivyo, amesema baada ya uharibifu huo Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa alifanya ziara Mkoani Morogoro, Pamoja na maeneo mengine alifika Wilayani Malinyi eneo lililoathirika na aliahidi kuleta fedha zitakazotumika kufanya matengenezo ya muda ya miundombinu hiyo wakati wanajipanga kwa ajili ya ujenzi wa kudumu.
Amesema, baada ya Waziri Mchengerwa kumwomba Dkt. Samia Suluhu Hassan fedha hizo na kuridhia, fedha hizo Shilingi 1.2 Bil. Tayari zilishaletwa na tayari zimefanya kazi ya kurejesha mawasiliano ndani ya Mji wa Malinyi.
Kwa sababu hiyo, Mhe. Adam Malima ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia fedha hizo za Matengenezo ya dharura kupelekwa Malinyi na kuwaletea wana malinyi mawasiliano yao huku akiwashukuru TANROADS kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Eng. Alinanuswe Lameck Kyamba amesema Serikali imeleta fedha fedha zilizotengwa kwa ajili ya dharura na kazi ya kurejesha mawasiliano imefanyika ndani ya wiki mbili na sasa wanajipanga kwa ajili ya matengenezo ya kudumu.
Nao wananchi wa Mji wa Malinyi akiwemo Thobias Ndombaheka na Francis Gerlad kwa niaba ya wananchi wenzao wamemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuwafungulia tena mawasiliano yaliyokuwa yameathiriwa na Mvua na sasa wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi bila usumbufu.
Barabara zilizofunguliwa ni pamojamna Barabara ya TARURA ya Malinyi – Igawa katika eneo la Kiwale Pamoja na Barabara ya TANROADS inayoingia Mjini Malinyi mbazo zote madaraja yake yalisombwa na maji ya mto Furua.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.