Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imewahakikishia wananchi juu ya upatikanaji wa Sukari nchini ambapo tayari shehena ya bidhaa hiyo tani 100000 imeshaingia nchini huku ikibainisha kuwa sukari hiyo itauzwa kwa bei elekezi kati ya shilingi 2,700 hadi 3,200 kwa kilo.
Serikali imebainisha hayo Hayo Januari 29, mwaka huu na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (MB) wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Biashara, Viwanda, Kilimo na Mifugo ilipotembelea kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichopo Wilayani Kilosa Mkoani humo.
Mhe. Silinde amekili kuwepo kwa uhaba wa sukari nchini unaotokana na viwanda kushindwa kuzalisha kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini na kusababisha bei ya sukari kupanda, hata hivyo amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua kudhibiti changamoto hiyo kwa kuagiza tani 100000 za sukari ambapo itauzwa kwa bei elekezi ili kila mwananchi aweze kumudu.
“...niwaambie tu wananchi Meli zimeshafika pale bandarini zipo kwenye maandalizi ya kushusha mzigo na sukari iliyoagizwa nchini na itauzwa kwa bei elekezi kati ya shilingi 2,700 na 3,200 kama ambavyo Bodi ya Sukari ilitoa...” amesema Mhe. Silinde.
Aidha, amesema Wizara imejiwekea mikakati ya muda mrefu na mfupi ambapo mkakati wa muda mrefu ni pamoja na kuondoa kabisa changamoto ya uhaba wa sukari nchini kwa kuongeza uzalishaji katika Viwanda vya sukari huku mkakati wa muda mfupi ni kuagiza sukari nje ya nchi hususan katika kipindi ambacho viwanda havizalishi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Biashara, Viwanda, Kilimo na Mifugo Mhe. Deo Mwanyika (Mb) amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia changamoto zinazopelekea kushuka kwa uzalishaji wa sukari nchini katika viwanda mbalimbali huku akithibitisha kuwa kweli mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimeongezeka kutoka mililita 200 hadi mililita 760 zimesababisha miundombinu ya barabara za mashamba na mashamba yenyewe kujaa maji hivyo kupelekea shughuli za uzalishaji sukari kusua sua.
Aidha, ameitaka Serikali kuhakikisha kuwa sukari iliyoagizwa kutoka nje inawafikia wananchi kwa bei elekezi ambayo imepangwa ili kuwaondolea wananchi malalamiko ya kupanda kwa kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo.
Kiwanda cha sukali cha Mkulazi hadi sasa kimezalisha zaidi ya tani 500 za sukari ambapo hivi karibuni zitaingizwa sokoni kwa ajili ya matumizi
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.