Serikali imewatahadharisha wananchi waishio maeneo ya mabondeni kuhama ili kuepuka athari za Mvua za Elnino zinazotarajiwa kunyesha kuanzaia mwezi Oktoba mwaka huu kama ilivyoelezwa kwenye taarifa ya Mamlaka ya Hali ya hewa Nchini (TMA).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe, Ummy Hamis Ndeliananga Septemba 25, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha kuimarisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kilichokuwa na lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya Elnino.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ummy ameitaka Mikoa na Halmashauri zote hapa nchini kuwa na mipango ya utekelezaji katika maeneo yao katika kukabiliana na mvua za Elnino lakini kwa kuzingatia Mipango ya Taifa iliyotolewa kwao.
“Mikoa na halmashauri iandae mipango ya utekelezaji katika maeneo yao kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Nino”. Amesema Naibu Waziri.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Sebastian Waryuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kusafisha mitaro ya kupitisha maji katika maeneo yao hususan katika kipindi hiki cha mvua ili kuepuka mafuriko yatayosabiabisha magonjwa ya mlipuko.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya kwa niaba ya MKuu wa Mkoa amewataka wananchi Mkoani humo wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama makazi yao Kwenda maeneo ya miinuko kwani amesema kinga ni bora kuliko tiba.
Akiwasilisha wasilisho lake katika kikao hicho, Meneja wa TMA kanda ya mashariki Bi. Hidaya Senga amewashauri wananchi kupata taarifa za hali ya hewa kupitia njia mbalimbali lakini zilizothibitishwa na TMA kwa kuwa taasisi hiyo ndiyo pekee hapa nchini yenye mamlaka ya kutoa taarifa hiyo.
Sambamba na hilo Bi Hidaya amewaomba waandishi wa Habari kutoa taarifa za hali ya hewa zile zilizohuishwa na Mamlaka ya Hali ya hewa Nchini kwa kutumia lugha rahisi, yenye kueleweka na bila kuleta mtafaruku kwa jamii.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Goodluck Zelote amesema tayari jeshi hilo limeuchukua hatua za mapema kukabiliana na janga la Elnino ikiwemo kuainisha maeneo Korofi yanayopata mafuriko mara kwa mara, kuandaa vifaa vya uokozi, kuandaa rasilimali watu Pamoja na kutoa elimu kwa wanachi namna ya kujikinga na mafuriko.
Kwa mujibu wa utabiri wa Mamlaka ya hali ya hewa Nchini mikoa 14 itakayoathirika na mvua hizo zitakazoanza kunyesha Oktober mwaka huu hadi Mwezi Januari 2024 ni Pamoja na Mkoa wa Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.