Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kukuza uchumi wa nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi zikiwemo taasisi za kidini kama Kanisa katoliki Jimbo la Morogoro kujikita katika shughuli za kiuchumi hususan Kilimo, Utalii, Elimu, Mawasiliano na huduma ya afya kwa manufaa ya wananchi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Muhagama katika ibada ya Shukrani ya kutimiza miaka 25 ya upadri wa Mhashamu Askofu Lazarus Vitalis Msimbe wa Jimbo katoliki la Morogoro iliyofanyika kwenye viwanja vya misionari ya mtakatifu Peter iliyopo kata ya Kilakala katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
"...Jimbo hili limeendelea kushiriki katika maendeleo mengi katika jamii ambapo mpo kwenye sekta ya Afya, Elimu, Mawasiliano na sekta nyingine nyingi..." amesema Mhe. Jenista Muhagama
Mhe. Muhagama amesema taasisi za kidini zinaombwa kuwekeza katika huduma mbalimbali ikiwemo Elimu, Kilimo, afya na nyingine nyingi kwani Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amejizatiti kushirikiana na taasisi hizo kupunguza vifo visivyokuwa na lazima ili kuwa na nguvu kazi ya uhakika hapa nchini.
Aidha, Mhe. Muhagama amewataka wazazi/walezi kuiga mfano wa wazazi wa Askofu Lazarus Vitalis Msimbe kuwalea watoto wao kwa kuzingatia utamaduni, Mila na desturi za nchi kwani utandawazi una mifumo inayoweza kuharibu watoto sambamba na vijana ambao ndio tegemeo la Taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewatahadharisha watanzania kuhusu mvua za El-nino baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa utabiri wa mvua hizo, hivyo amesema ni jukumu la watanzania wote kushirikiana ili kukabiliana na maafa pale yatakapojitokeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema inatakiwa taasisi za kidini ikiwemo kanisa katoliki la Morogoro kuendelea kuwekeza katika shughuli za kiuchumi hususan katika Utalii na Kilimo ambapo amebainisha mazao ya kibiashara yakiwemo karafuu, hiliki, Kakao yanayolimwa Mkoani humo na kuahidi Ofisi yake ya Mkoa kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo kama itahitaji kuwekeza katika kilimo hicho.
Sambamba na hilo, Mhe. Malima amesema Kanisa hilo liendelee kukemea ukatili wa watoto, mauaji ya vikongwe na albino sambamba na kukemea ndoa za jinsia moja kwani hukwamisha shughuli za maendeleo ambapo ndio chachu ya kukuza uchumi wa Taifa.
Nae, Mhashamu Askofu Lazarus Vitalis Msimbe wa Jimbo katoliki la Morogoro pamoja na kutoa shukrani zake kwa wote waliohidhuria ibada hiyo ameitaka jamii kumtegemea Mungu na kutenda matendo mema kwa jirani na jamii kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.