Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Bw. Anza-Ameni Ndosa amesema wanajivunia mafanikio ya program Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT – MMMAM) ambayo imewajengea watoto Mkoani humo mazingira mazuri ya kujifunzia, upatikanaji wa lishe bora na kuwawezesha wazazi na walezi kutoa malezi bora.
Anza-Ameni Ndosa amesema hayo Agosti 29, 2023 wakati akifungua kikao cha mapitio ya utekelezaji wa Programu hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Amesema Serikali ilianzisha programu hiyo mwaka 2021 ambayo inatekelezwa katika Mikoa 26, Mkoa wa Morogoro ukiwa miongoni mwa mikoa hiyo kwa kushirikiana na shirika la Childhood Development Organization (CDO) kutekeleza programu hiyo katika Halmashauri zote 9 za Mkoa huo na kubainisha kuwa hiyo imehamasisha watoto kupata chakula wakiwa shuleni na kusaidia idadi ya watoto wanaojiunga na elimu ya awali kuongezeka.
“...tunajivunia mafanikio tuliyoyapata hadi sasa na tutaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa kila mtoto katika Mkoa wa Morogoro anapata fursa sawa na kuanza maisha yao wakiwa na msingi imara...tutaendelea kufanya kazi na wadau ili kuendeleza programu hii...” amesema Bw. Ndosa.
Akielezea lengo la Programu MMMAM ambayo ilizinduliwa Mkoani humo Mei 23, 2023, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Morogoro Bi. Delfina Pacho amesema, lengo programu hiyo ni kuondoa changamoto za watoto walio chini ya miaka 8 na kikao hicho kinajadili utekelezaji wa programu ngazi ya Mkoa na Halmashauri ili kubaini mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa programu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Childhood Development Organization (CDO) Bi. Felistas Kalomo amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmshauri za Mkoa wa Morogoro kutekeleza agizo la Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mhe. Dkt. Dorothhy Gwajima (Mb) lililotaka kufungia vituo vyote vya kulea watoto mchana (Day Care) ambavyo havijasajiliwa na havikidhi vigezo vya kupokea watoto.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.