Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga Tsh. bilioni 100 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa vyuo 64 vya fundi stadi ngazi ya Wilaya na chuo kimoja cha ufundi cha Mkoa wa Songwe.
Mhe. Omari Kipanga Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akizungumza na washiriki mbalimbali wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watekelezaji wa mafunzo ya mradi wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi.
Hayo yamebainishwa Machi 10, 2023 mwaka huu na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Juma Kipanga (MB) wakati akifungua mafunzo kwa watekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF.
“…mwaka 2022/2023 serikali imetenga bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo stadi 64 katika ngazi ya wilaya na Chuo kimoja katika Mkoa wa Songwe, yaani katika Mikoa 26 ya Tanzania bara, Mikoa 25 tayari tumeshajenga isipokuwa Mkoa mmoja ambao ni Mkoa wa Songwe ambapo kwa bajeti hii ya 2022/2023 tunakwenda kujenga chuo hicho…” amesema Mhe. Omari Juma Kipanga.
Washiriki wa mafunzo kwa watekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi wakimsikiliza Mhe. Omari kipanga Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
Aidha, Mhe. Kipanga amesema lengo kuu la serikali kujenga vyuo hivyo ni kutaka vijana wa kitanzania kuwa na uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa, kuondoa changamoto ya ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kipanga amewataka watekelezaji hao kukamilisha ujenzi wa majengo 9 kwa Kila Wilaya ifikapo mwezi Septemba Mwaka huu kwa Ubora unaotakiwa na kwa kulinganisha na kiwango cha fedha kilichotolewa ( Value for money).
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa Bi. Germana Mung'aho amesema vyuo hivyo vitawasaidia vijana wa elimu mbalimbali ili kukuza maendeleo ya Morogoro na taifa kwa ujumla, hata hivyo amesema Mkoa wa Morogoro unatarajia kuwa na vyuo viwili vya ufundi stadi ambavyo bado vipo kwenye hat ha za ujenzi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia Mhe. Omari Juma Kipanga (Mb) (wa tatu kushoto waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali baada ya ufunguzi wa mafunzo kwa watekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.