Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa Shaka Hamdu Shaka ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro kuwawesheza vijana kupitia asilimia kumi (10%) ya fedha zinazotolewa na Serikali kwenye Halmashauri hapa nchini kwa ajili ya maendeleo ya Vijana, Wazee, Wanawake na wenye Ulemavu Ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Shaka Hamdu Shaka akiwa na baadhi ya viongozi wa Mkoa, wabunge na wakulima kwenye Shamba la Vijana wakati wa upandaji wa miche ya mikonge kwenye Shamba hilo.
Shaka Hamdu Shaka ametoa agizo hilo Oktoba 4 Mwaka huu akiwa mgeni rasmi katika tukio la kuzindua msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 uliofanyika katika Kijiji cha Lukwembe Kata ya Tindiga Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
".....Rai yangu sisi tunazo fedha, Vijana hawa lazima wawezeshwe kwa mitaji, Vijana hawa lazima wawekewe utaratibu mzuri wa kusimamiwa, lakini Vijana hawa lazima tuhakikishe kwamba wanaendelea na sio wanarudi nyuma, kuwapa maeneo ni jambo moja, kuwaendeleza ni jambo la pili...."
Aidha, ameongeza kuwa Sasa ni wakati wa viongozi kubadilika kimtazamo na kimawazo na badala yake fedha hizo zitumike kwa kuendelezwa kuliko maeneo ambayo fedha hizo zinapotea kutokana na ukosefu wa usimamizi mzuri hivyo madiwani wa Kilosa wanatakiwa wakasimamie fedha hizo ziwafikie vijana.
Uzinduzi huo umekwenda sambamba na upandaji wa zao la Mkonge katika shamba la vijana lenye ukubwa wa ekari 1,200 kutoka moja ya mashamba 11 yaliyofutwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa kwa wawekezaji na kurejeshwa kwa wananchi ili kupata ardhi ya kulima na kupunguza migogoro baina ya wakaulima na wafugaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Fatma Abubakar Mwassa akimkaribisha mgeni wake amebainisha namna Ofisi yake ilivyojipanga kutatua migogoro ya Ardhi baina ya wakulima na wafugaji kwamba tayari Serikali imedhamiria kujenga Kituo cha Polisi katika eneo baina ya pande hizo mbili hususan katika Kata ya Tindika na kwamba Polisi watahusika kwa karibu zaidi kusimamia pande hizo mbili kufanya shughuli zao bila adha yoyote.
Aidha, amesema shamba la vijana la Ekari 1200 litatumika kulima kwa mfumo wa Block farm na kujikita zaidi kulima zao la Mkonge huku eneo nyingine ambalo limeharibiwa na Mto serikali inafanya juhudi kulirejesha ili vijana wengi wapate fursa ya kushiriki kulima mboga mboga na mazao mengine katika eneo hilo.
Amesema lengo la Serikali ni kuzirudisha Ekari 3000 zilizoharibiwa na mto hivyo kuwa na jumla ya Ekari 6000 zitakazowawezesha vijana kujiajiri wenyewe na kujikita katika kilimo chenye tija.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa Profesa Paramagamba Kabudi amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufuta umiliki wa mashamba 11 na kuyarejesha kwa wananchi, huku akibainisha kuwa uamuzi huo ni wa kihistoria haijawahi kutokea kufuta idadi kubwa ya mashamba kama hayo kwa wakati mmoja.
Katibu Tawala Msaidizi- Uchumi na Uzalishaji akipanda ache wa mkonge kwenye Shanna la Vijana Makati wa uzinduzi wa msimu mpya wa kilimo 2022/2023 uliofanyika Wilayani Kilosa.
Hata hivyo Profesa Kabudi amewataka wananchi wa Wilaya ya Kilosa hususan wa Kata ya Tindiga ambapo mashamba hayo yapo, kutumia fursa hiyo kufanya kazi kwa bidii kwenye kilimo ili kujikwamua kiuchumi kupitia mashamba hayo yaliyofutwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.