SHIGELA AAGIZA MIRADI YA MAJI KUKAMILIKA HARAKA
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewaagiza Maafisa wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro (MORUWASA) pamoja na wakandarasi wanaosimamia Ujenzi wa matenki mawili ya maji yatakayohudumia kutoa maji maeneo ya Mkundi, Kihonda na Tungi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo.
Martine Shigela ametoa agizo hilo Juni 9 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kusikiliza kero za wananchi kwa Kata zote zilizoko katika Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (mwenye shati ya dhambarau) akitoa maelekezo kwa wahandisi na MORUWASA kama wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kusambaza maji kukamilisha mradi huo ndani wakati uliopangwa.
Aidha, Martine Shigela amesema Serikali katika kutatua changamoto hiyo tayari imetoa kiasi cha zaidi ya shilingi 1.5 Bil. ili kugharamia ujenzi wa matenki hayo na kituo kimoja cha kusambazia maji kwa wananchi wa maeneo hayo.
Shigela amebainisha kuwa ujenzi wa atenki kubwa la kuhifadhia maji upande wa Kihonda na Mkundi hadi kukamilika kwake litagharimu shilingi milioni 600, ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa maji lita 1mil. upande wa Tungi na Kilimanjaro limegharimu shilingi 467mil pamoja na ujenzi wa kituo cha pampu mbili za kusukuma maji kilichogharimu kiasi cha milioni 590.
“zaidi ya Tsh 1.6 Bil. zimeshatolewa kwa wakandarasi, hivyo ninaagiza kwa wakandarasi na MORUWASA kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili ndani ya mwaka huu wananchi waanze kupata huduma ya maji” ameagiza Shigela.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Hamashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga ameishukuru Serikali kwa jitihada za kutatua kero ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo kwani huduma ya maji kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi hao, hivyo kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia wananchi kuondokana na changamoto hiyo.
Naye meneja ufundi wa MORUWASA Mhandisi Victor Ngowi amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kukamilisha mradi huo wa maji kwa muda uliopangwa na kuahidi kufanya kazi hiyo usiku na mchana.
Mradi huo wa maji ambao unahusisha ujenzi wa matenki mawili ya maji na kiutuo cha kusukuma maji umeanza Machi 30 na unatarajia kukamilika Juni 30 mwaka huu lengo ni kuharakisha kukamilika kwake ili kutatua kero hiyo ya maji kwa wananchi wa maeneo ya Mkundi, Kihonda na Tungi.
Muonekano wa kituo cha kusambaza maji kilichopo Kihonda Mizani ambapo kilikaguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Juni 9 Mwaka huu wakati ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.