Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani humo kuhakikisha anajiridhisha na uimara wa madaraja na makaravati yote ya Mkoa huo kuwa yako salama kabla ya msimu wa mvua haujawadia.
Martine Shigela ametoa agizo hilo Oktoba 5, mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku moja Wilayani Kilosa iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kutatua kero za wananchi katika Tarafa ya Magole.
Mradi wa kwanza alioutembelea Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa ziara hiyo ni pamoja na ujenzi wa daraja la Kiegea lililoanza kujengwa rasmi Novemba 5, mwaka jana kazi ambayo ilitarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita na kushindwa kukamilika kutokana na sababu mbalimbali.
Akiwa katika mradi huo pamoja na kupongeza hatua iliyofikiwa ya asilimia 90 ya ujenzi wa daraja hilo, alimtaka mkandarasi kukamilisha kazi hiyo kwa muda ulioongezwa huku akitumia fursa hiyo kumuagiza Meneja wa TANROADS kupitia madaraja na makaravati yote ya Mkoa huo kuyafanyia matengenezo yanayohitaji kukarabatiwa kabla ya msimu wa mvua haujaaza.
“kwa hiyo nimekuja kufanya ukaguzi, tunaelekea masika na nimuelekeza Meneja wa TANROADS matatizo tuliyoyapata mwaka jana tusiyapate mwaka huu, kwa hiyo tujiridhishe madaraja yote na makaravati yote toka mpakani mwa Pwani mpaka mpakani mwa Dodoma tuyapitie makaravati yote na kutoka mpakani mwa Pwani mpaka mpakani mwa Iringa…..aliagiza Martine Shigela.
Akifafanua kuhusu umuhimu wa barabara na watumiaji wake, Shigela amesema barabara zinaposimama kwa sababu ya ubovu kimsingi zinasimamisha Uchumi wa eneo husika na wa taifa nzima kwani watu mbalimbali hawatafanya kazi wakiwemo madereva, watu wa Bandarini, wauza mafuta, nyumba za wageni na wafanyabiashara wengine watasimama kufanya kazi na kusababisha madhara makubwa kwa nchi kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Martine Shigela amempongeza Mkandarasi anayejenga daraja la Kiegea Eng. Aloyce Stephen ambaye ni mzawa, kwa kutekeleza kazi hiyo kwa uaminifu huku akiwataka wakandarasi wengine wazawa kuiga mfano wa Mkandarasi huyo kufanya kazi kwa uzalendo ili kuondoa dhana iliyojengeka kuwa wakandarasi wazawa hawawezi kufanya kazi zao kikamilifu mara wanapopewa tenda hizo.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa daraja hilo la Kiegea ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu shilingi za kitanzania Bil. 6.9 Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Eng. Baraka Mwambage alimueleza Mkuu wa Mkoa sababu zilizokwamisha ujenzi huo kuchelewa zikiwemo za kiufundi na wingi wa mvua, kwani mwezi mmoja baada ya kuanza kazi hiyo zilianza kunyesha.
Hata hivyo Eng. Mwambage alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa ujenzi wa daraja hilo utakamilika ndani ya wiki mbili zijazo yaani kabla ya mwezi Novemba mwaka huu magari yote yataanza kupita juu ya daraja hilo la Kiegea.
Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo Eng. Aloyce Stephen alieleza changamoto iliyomfanya kuchelewa kukamilisha kazi ya ujenzi huo kuwa ni kutokana na baadhi ya vifaa vya ujenzi kuchelewa kuletwa eneo la ujenzi kutoka Dar es Salaam huku akimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa kazi hiyo itakamilika kabla au ifikapo Oktoba 30 mwaka huu.
Akiwa katika kata ya Berega Mkuu wa Mkoa alikagua ubovu wa Daraja la Beraga ambalo mara kadhaa limeleta adha kwa wananchi hususan akinamama wanaokwenda kupata matibabu katika hospitali ya Berega.
Diwani wa kata ya Berega Elikana Masonda kwa niaba ya wananchi alieleza adha wanayopata wananchi wake kipindi cha masika hususan wananwake wanapokwenda kupata huduma za Afya katika hospitali ya Berega hulazimika kusubiri maji yaliyojaa kupungua ndipo waendelee na safari jambo ambalo ni usumbufu kwa wagonjwa na akina mama.
Hata hivyo Diwani huyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa Tsh. Bilioni 7.9 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambao linatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ametembelea Kata tatu za Mtumbatu na Dumila ambako alifanya mikutano ya hadhara na kutatua kero za wananchi pamoja na kata ya Berega ambako alitembelea madaraja hayo mawili ya Kiegea na daraja la Berega.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.